Magaidi 100 wa Daesh wauawa katika mashambulio ya anga nchini Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i15055-magaidi_100_wa_daesh_wauawa_katika_mashambulio_ya_anga_nchini_iraq
Wanachama wasiopungua 100 wa kundi la kigaidi la Daesh wameuawa nchini Iraq kufuatia mashambulio ya anga yaliyofanywa na ndege za kijeshi za nchi hiyo katika mkoa wa al-Anbar magharibi mwa nchi hiyo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Sep 10, 2016 09:34 UTC
  • Magaidi 100 wa Daesh wauawa katika mashambulio ya anga nchini Iraq

Wanachama wasiopungua 100 wa kundi la kigaidi la Daesh wameuawa nchini Iraq kufuatia mashambulio ya anga yaliyofanywa na ndege za kijeshi za nchi hiyo katika mkoa wa al-Anbar magharibi mwa nchi hiyo.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq imetangaza kuwa, ndege za kijeshi za nchi hiyo zimefanya mashambulio kadhaa katika maeneo ambayo ni ngome za kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika mkoa wa al-Anbar na kupelekea wanachama 100 wa kundi hilo kuuawa.

Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa, miongoni mwa waliouawa wamo makamanda wa ngazi za juu wa kundi hilo la kigaidi ambalo linasifika kwa kutenda jinai za kutisha.

Wapiganaji wa kujitolea wa jeshi la wananchi la  "al-Hashd al-Shaabi"

Sehemu nyingine ya taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq imeeleza kwamba, mashambulio hayo ya anga yamepelekea pia kiwango kikubwa cha silaha na zana za kivita za magaidi hao wa Daesh kuharibiwa.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Ijumaa ya jana watu wasiopungua 35 waliuawa mjini Baghdad baada ya kutokea mlipuko wa bomu lililotegwa na magaidi wa Daesh mbele ya jengo la Wizara ya Mafuta.

Katika siku za hivi karibuni wanajeshi wa Iraq wakishirikiana na jeshi la kujitolea na wananchi wamefanikiwa kuyakomboa maeneo mengi ya nchi hiyo yaliyokuwa yakidhibitiwa na kundi la kigaidi la Daesh.