Iran: Madai kuwa Tehran inaipa silaha Ansarullah ya Yemen haya msingi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i16324-iran_madai_kuwa_tehran_inaipa_silaha_ansarullah_ya_yemen_haya_msingi
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha vikali madai yaliyotolewa na Saudi Arabia kuwa Tehran inalifadhili kundi la wanaharakati wa Ansarullah wa Yemen.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 29, 2016 13:46 UTC
  • Iran: Madai kuwa Tehran inaipa silaha Ansarullah ya Yemen haya msingi

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha vikali madai yaliyotolewa na Saudi Arabia kuwa Tehran inalifadhili kundi la wanaharakati wa Ansarullah wa Yemen.

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameliandikia barua Baraza la Usalama la umoja huo akipinga madai hayo na kusisitiza kuwa hayana msingi. Barua ya mwanadiplomasia wa Iran ni radiamali kwa barua iliyoandikwa na Saudia kwa Baraza la Usalama mnamo Septemba 16, ikidai kuwa Jamhuri ya Kiislamu inawatumia silaha wanaharakati wa Ansarullah wa Yemen. Kadhalika Gholam Ali Khoshro, Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amebainisha katika barua yake kwa Baraza la Usalama kuwa, utawala wa Riyadh ndio unaotumia silaha zake nzito dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen katika hujuma zake.

Athari za hujuma ya Saudia nchini Yemen

Tangu ulipoanzisha uvamizi wake wa kijeshi dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka 2015 hadi sasa muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia na kuungwa mkono na Marekani umeshazishambulia skuli, hospitali, makaazi ya raia, misikiti na kambi za wakimbizi na kuua maelfu ya raia wasio na hatia wa nchi hiyo.

Askari vamizi wa Saudia nchini Yemen

Zaidi ya watu 10,000 wamepoteza maisha katika hujuma ya kinyama ya Saudia dhidi ya Yemen inayolenga kumrejesha madarakani kibaraka wake, rais mtoro na  aliyejiuzulu wa nchi hiyo Abd Rabu Mansour Hadi na kuwaondoa madarakani wanamapinduzi wa Ansarullah.