Hamas yaikosoa ICC kwa kutoutembelea Ukanda wa Gaza
(last modified Sun, 09 Oct 2016 08:18:44 GMT )
Oct 09, 2016 08:18 UTC
  • Hamas yaikosoa ICC kwa kutoutembelea Ukanda wa Gaza

Harakati ya muqawama wa Palestina Hamas imesema safari ya ujumbe wa maafisa wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu haina maana na umuhimu wowote, madhali wataalamu hao wa masuala ya sheria watakosa kuutembelea Ukanda wa Gaza.

Taarifa iliyotolewa na Hamas imesema uamuzi wa timu hiyo ya ICC kukosa kuitembelea Gaza umechochewa moja kwa moja na utawala haramu na wa Kizayuni wa Israel.

Timu hiyo ya wataalamu wa ICC ikiongozwa na mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo Fatou Bensouda, iliwasili katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu Jumatano iliyopita na inatazamiwa kukamilisha safari hiyo kesho Jumatatu.

Wanamapambano wa Hamas

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imesema badala ya safari ya wajumbe wa ICC katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kuwa ahueni na kuleta matumaini kwa Wapalestina, imekuwa ni sawa na kutia chuma moto kwenye kidonda kwa familia za wahanga wa jinai za utawala haramu wa Israel.

Ujumbe huo umezitembelea Tel Aviv, Quds Tukufu na mji wa Ramallah, ulioko kati kati mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huku ukikosa kuutembelea Ukanda wa Gaza, ambao umekuwa chini ya mzingiro kwa takriban muongo mmoja sasa.

Watoto ndio wahanga wakuu wa hujuma za Israel huko Gaza

Hii ni licha ya kuwa mahakama hiyo ya kimataifa ilisema kuwa mojawapo ya malengo ya safari hiyo yake ni kuchunguza uvamizi wa kijeshi wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Gaza mwaka 2014, ambapo Wapalestina 2,200 wakiwemo watoto wadogo zaidi ya 500 waliuawa shahidi na askari katili wa Israel.

Ukanda wa Gaza wenye takriban watu milioni 2 umekuwa chini ya mzingiro wa kibaguzi na kidhalimu wa utawala wa Kizayuni wa Israel tangu mwezi Juni mwaka 2007 na kuyafanya maisha ya Wapalestina wanaoishi katika ukanda huo kuwa magumu.

Tags