Mivutano katika uhusiano wa Misri na Saudia
Inavyoonesha, mgogoro wa Syria utaifanya fungate ya ndoa ya uhusiano wa Misri na Saudi Arabia imalizike kabla ya muda uliotarajiwa.
Serikali ya Misri imeuunga mkono mpango wa Russia kuhusu hali ya mambo ya Syria lakini Abdullah al-Muallemi, balozi wa Saudi Arabia katika Umoja wa Mataifa ameikosoa Misri na kuuelezea mpango huo wa Moscow kuwa ni wenye kuumiza. Mara baada ya kubainishwa misimamo hiyo ya Cairo na Riyadh imetangazwa kuwa shirika la mafuta la Saudi Arabia la Aramco, ambalo ni shirika kubwa zaidi la mafuta duniani limekusudia kusimamisha misaada ya mafuta ya Saudia kwa Misri. Aidha inasemekana kuwa kanali ya televisheni ya Al-Arabiyya inayomilikiwa na utawala wa Aal Saud itasitisha kuendesha shughuli zake nchini Misri kutokana na mikwaruzano iliyozuka katika uhusiano wa nchi hiyo na Saudia.
Misri ni nchi kubwa zaidi ya Kiarabu, lakini kwa muda sasa imepoteza nafasi yake hiyo ya kuwa dola lenye nguvu zaidi na kiongozi wa Ulimwengu wa Waarabu. Na sababu kuu ya hali iyo ni kuongezeka matatizo ya kiuchumi yanayoikabili Misri ambayo serikali ya sasa ya nchi hiyo ya Abdel Fattah el-Sisi nayo pia inakabiliana nayo.
Baada ya El Sisi kuingia madarakani, mahitaji ya kiuchumi ya Misri na utashi wa kisiasa wa Saudia hususan upinzani wake dhidi ya harakati ya Ikhwanul Muslimin sambamba na nia ya Riyadh ya kuzuia usitokee mparanganyiko katika mlingano wa nguvu za kisiasa katika eneo uliufanya utawala wa Aal Saud uwe na hamu ya kuimarisha uhusiano wake na utawala mpya wa Cairo.
Wakati mapinduzi ya kijeshi yalipotokea Misri mwaka 2013, Saudi Arabia ilikuwa nchi ya kwanza kuyatambua rasmi mapinduzi hayo ya kijeshi yaliyofanywa dhidi ya serikali halali ya Muhammad Morsi na kutuma salamu za pongezi kwa serikali mpya iliyoingia madarakani. Hata ukatili na umwagaji damu wa Agosti 2013 uliofanywa na utawala wa kijeshi dhidi ya wafuasi wa Morsi na kusababisha kuuawa na kujeruhiwa maelfu ya Wamisri uliitwa na utawala wa Riyadh kuwa ni "mapambano ya kupiga vita ugaidi".
Wiki moja tu baada ya mapinduzi ya kijeshi ya Misri, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) au Imarati na Kuwait ambazo kiuchumi ni nchi tatu za kibepari za Baraza la Ushirikiano ya Ghuba ya Uajemi zilitoa ahadi ya kuisaidia kiuchumi Misri kwa kuipatia dola bilioni 12 kwa njia ya mkopo, amana na bidhaa za mafuta. Misaada ya kifedha ya Saudia, Imarati na Kuwait iliwezesha akiba ya fedha za kigeni ya Benki Kuu ya Misri kuongezeka kwa kiwango cha dola bilioni 18.9 mnamo mwezi Agosti mwaka 2013 ambacho kilikuwa kiwango cha juu zaidi tokea mwaka 2011 na kuendelea. Mwezi Novemba 2013 vyombo vya habari viliripoti kuwa Saudia na Imarati zimedhamini muamala wa silaha wenye gharama ya dola bilioni mbili kati ya Misri na Russia. Na baada ya hapo pia misaada ya aina hiyo kwa serikali ya Abdel Fattah es Sisi iliendelea.
Hatua nyingine iliyochukuliwa na Utawala wa Aal Saud kuisaidia na kuiunga mkono serikali ya el Sisi ilikuwa ni ya Januari mwaka 2014 ambapo Saudia ikishirikiana na Imarati na Kuwait iliiweka harakati ya Ikhwanul Muslimin kwenye orodha moja ya makundi ya kigaidi pamoja na Al Qaeda na Jabhatu-Nusra na kuitangaza rasmi harakati hiyo kongwe ya Kiislamu nchini Misri kuwa ni kundi la kigaidi.
Kutokana na hatua zote hizo, mara baada ya Jenerali Abdel Fattah el Sisi kushika hatamu za madaraka, safari yake ya kwanza aliyofanya nje ya nchi mnamo Julai 2014 ilikuwa ya kuitembelea Algeria na safari yake ya pili ya mwezi Agosti mwaka huo huo ilikuwa ya nchini Saudi Arabia. Mnamo mwaka uliopita pia el Sisi alifanya safari mara mbili kuelekea Saudia ambako alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo. Mara baada ya Abdel Fattah el Sisi kuwa rais wa Misri viongozi wa utawala wa Aal Saud nao pia wamefanya safari mara kadhaa nchini Misri ikiwemo ya mwezi Aprili mwaka huu aliyofanya Mfalme Salman bin Abdulaziz huko mjini Cairo.
Hata hivyo licha ya kustawisha uhusiano wao wa pande mbili kwa kiwango hicho, Misri na Saudia zina hitilafu kubwa katika masuala ya kieneo hususan mgogoro wa Syria. Japokuwa serikali ya Misri inashiriki katika muungano wa kivita wa nchi za Kiarabu unaoongozwa na Saudia katika uvamizi na hujuma dhidi ya Yemen lakini ushiriki huo ni wa kiwango fulani tu; na kama wanavyoeleza baadhi ya wachambuzi, Misri inashiriki katika vita hivyo ili tu iweze kuendelea kupata misaada ya kiuchumi ya Saudia.
Hitilafu kubwa zilizopo kati ya Cairo na Riyadh ni kuhusu mgogoro wa Syria. Baada ya el Sisi kuingia madarakani Cairo imesisitiza mara kadhaa kuwa mgogoro wa Syria ni suala la ndani na hautotatuka kwa uingiliaji wa madola ya kigeni; na hapo ndipo inapotafautiana mno na utawala wa Riyadh.
Hitilafu hizo kuhusiana na mgogoro wa Syria ndizo zilizoifanya serikali ya el Sisi iupigie kura ya ndiyo mpango uliopendekezwa na Russia kuhusu mgogoro huo; jambo ambalo halikuifurahisha serikali ya Riyadh. Ukweli ni kwamba japokuwa serikali ya Misri inaihitajia Saudia kutokana na matatizo ya kiuchumi iliyonayo lakini matatizo hayo hayawezi kuisahaulisha enzi zake za kujivunia na kukubali kuburuzwa kwa sababu ya ghururi na tabia ya kupenda jaha ya utawala wa Saudia ambao baadhi ya watawala wake ni wanagezi mno wa siasa kiasi kwamba kulitaja jina tu la mtu kama Jamal Abdulnasir wa Misri, kwao wao ni jambo la fahari na kujivunia.../