Iraq yamjibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq imeyataja matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia dhidi ya vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Iraq kuwa hayana maana na kusema kwamba, vikosi hivyo ni fakhari kwa Wairaqi.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq leo imesisitiza kuwa matamashi yaliyotolewa na Adel al Jubair Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia dhidi ya vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Iraq yanayonyesha chuki ya Saudia kwa Iraq na hasira za nchi hiyo mbele ya ushindi unaopata vikosi hivyo dhidi ya magaidi.
Katika hatu ambayo inaonekana wazi ni kuingilia mambo yasiyomuhusu, Adel al Jubair Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia jana alidai kuwa vikosi vya Hashdu al Sha'abi vya wananchi wa Iraq vimekusudia kuleta mgawanyiko wa kitaifa.
Al Jubair aliingilia waziwazi maamuzi ya wananchi wenyewe wa Iraq mjini Riyadh jana Alkhamisi mbele ya waandishi wa habari akiwa pamoja na Mevlut Cavusoglu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki. Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia na mwenzake wa Uturuki walifanya mkutano huo na waandishi wa habari pambizoni mwa kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi Wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi.