Mbunge: Uwezekano wa Misri kukata uhusiano na Saudia ni mkubwa
Mbunge mmoja nchini Misri ameonya kuwa uwezekano wa Cairo kukata uhusiano wake na Saudi Arabia ni mkubwa sana na kusisitiza kuwa iwapo nchi mbili hizo zitakata uhusiano wao, itakuwa ni kwa manufaa na maslahi ya Ulimwengu wa Kiarabu.
Amin Iskander, mbunge wa Chama cha Al-Karama na muasisi wa harakati ya Kefaya ameliambia shirika la habari la Tasnim kuwa, kuna haja kwa Misri kukata uhusiano na 'utawala ulioanzisha ugaidi duniani wa Riyadh.'
Ameongeza kuwa, hatua ya watawala wa Misri kufuata kibubusa sera za Saudia imeathiri pakubwa ushawishi na nafasi ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika katika bara hilo na eneo la Mashariki ya Kati. Mbunge huyo wa Misri amesema Riyadh imekuwa ikijipiga kifua na kujinadi kuwa ni dola lenye nguvu katika eneo na kusisitiza kuwa utawala huo wa kifalme hauna itibari na haiba ya kuwa na ushawishi katika eneo kama Iran.
Uhusiano kati ya Cairo na Riyadh umeendelea kutikisika, baada ya Misri kupiga kura ya ndio kuunga mkono azimio la Russia katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, linalotaka kuendelea mashambulizi ya anga katika eneo la Aleppo nchini Syria, dhidi ya makundi ya kigaidi na kitakfiri.
Hii ni katika hali ambayo, siku chache zilizopita, mashirika ya utalii nchini Misri yalisimamisha safari za ndege za wafanya ziara ya ibada ya Umrah nchini Saudia kutokana na hatua ya Riyadh kuongeza gharama za viza ya kuingia nchini humo kwa mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu.