Oct 20, 2016 07:49 UTC
  • HAMAS yalaani msimamo wa Katibu Mkuu wa UN dhidi ya UNESCO

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imemkosoa vikali Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kuunga mkono sera za kujipanua za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Hamas imetoa taarifa ya kulaani matamshi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki moon ya kukosoa azimio lililopitishwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la umoja huo UNESCO kuhusiana na msikiti mtukufu wa Al-Aqsa.

Harakati hiyo ya muqawama wa Kiislamu ya Palestina imesisitiza kuwa matamshi hayo ya Ban Ki moon ni sawa ni kujivua wajibu wake wa kuwakilisha msimamo na maazimio rasmi ya taasisi za Umoja wa Mataifa na vile vile ni dhihirisho la kukiuka sheria za kimataifa kwa ajili ya kukidhi manufaa na maslahi ya utawala haramu wa Israel.

Waislamu wa Palestina wakisali katika eneo la misikti wa Al-Aqsa

Siku ya Jumanne, Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa anayemaliza muda wake alikosoa hatua ya Shirika la umoja huo la Elimu, Sayansi na Utamaduni ya kupitisha rasmi azimio kuhusu msikiti mtukufu wa Al-Aqsa. Kupitia azimio hilo, UNESCO imetangaza rasmi kuwa kibla hicho cha kwanza cha Waislamu ni turathi ya Kiislamu tu.

Kwa mujibu wa azimio lililopitishwa rasmi na Baraza la Utendaji la UNESCO hakuna uhusiano wowote wa kidini baina ya msikiti mtukufu wa Al-Aqsa na Mayahudi, na msikiti huo ni mahala patakatifu kwa Waislamu. 

Al-Aqsa ni msikiti wa tatu kwa utukufu katika Uislamu baada ya Msikiti mtukufu wa Makka na Msikiti wa Mtume Muhammad SAW wa mjini Madina.

Hata hivyo Ban Ki moon amedai kuwa sehemu ya kale ya mji wa Baitul Muqaddas na kuta zake ni milki ya pamoja ya dini tatu za tauhidi za Uislamu, Ukristo na Uyahudi.../

Tags