Al-Wefaq: Wabahrain wataendelea kuiunga mkono Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i17821-al_wefaq_wabahrain_wataendelea_kuiunga_mkono_palestina
Chama cha Kiislamu cha al-Wefaq cha Bahrain kimesema hakuna nafasi ya utawala wa Kizayuni wa Israel nchini humo na kusisitiza kuwa wananchi wa Bahrain wataendelea kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina.
(last modified 2026-02-25T07:04:48+00:00 )
Oct 20, 2016 14:00 UTC
  • Al-Wefaq: Wabahrain wataendelea kuiunga mkono Palestina

Chama cha Kiislamu cha al-Wefaq cha Bahrain kimesema hakuna nafasi ya utawala wa Kizayuni wa Israel nchini humo na kusisitiza kuwa wananchi wa Bahrain wataendelea kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina.

Sheikh Hussein al-Daihi, Katibu Mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani Bahrain ameyasema hayo baada ya serikali ya Manama kukubali kuwa mwenyeji wa ujumbe wa maafisa wa utawala haramu wa Israel mwaka ujao.

Katibu Mkuu wa al-Wefaq amesema wananchi wa Bahrain katu hawatoacha njia ya kuiunga mkono Palestina na kutetea kibla cha kwanza cha Waislamu cha al-Aqsa na kwamba uamuzi wa watawala wa Manama wa kuwakaribisha nchini humo maafisa wa utawala ghasibu wa Israel haumaanishi kuwa umepata baraka za wananchi wote wa Bahrain.

Maandamano ya wananchi wa Bahrain dhidi ya serikali sambamba na kushinikiza kuachiwa huru wanazuoni wa Kiislamu

Rais wa Shirikisho la Soka Bahrain, Ali bin Khalifah Aal Khalifah hivi karibuni alisema utawala wa Manama umeidhinisha kwenda nchini humo maafisa wa utawala wa Israel, kushiriki kongamano la Shirikisho la Soka Duniani FIFA mwezi Mei mwakani. 

Ni vyema kukumbusha kuwa, mwezi Julai mwaka huu, mahakama moja nchini Bahrain ilikivunja chama cha al-Wefaq, mwezi mmoja baada ya serikali ya Manama kusimamisha shughuli za chama hicho.

Aidha mahakama hiyo iliagiza kuzuiliwa fedha na mali zote zinazomilikiwa na chama hicho cha Kiislamu. Hatua hiyo ya utawala wa ukoo wa Aal Khalifa ilikosolewa vikali na mashirika mbali mbali ya kutetea hazi za binadamu duniani pamoja na baadhi ya nchi ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.