Mash'al: Kuna udharura wa kufikiwa umoja wa kitaifa Palestina
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema kuwa upo udhaura wa kufikiwa umoja wa kitaifa wa Palestina ili kukomesha ukaliaji mabavu wa Israel.
Khalid Mash'al amesema kuwa upo ulazima wa kushirikishwa makundi yote, kufikiwa umoja wa kitaifa, kuwekwa kando hitilafu na misimamo ya undumakuwili kwa minajili ya kuipatia ufumbuzi hali ya mambo ya ndani ya Palestina na pia kukomesha ukaliaji mabavu wa adui Mzayuni.
Khalid Mash'al ameongeza kuwa wananchi wa Palestina wanaendeleza jitihada za kusogeza mbele muqawama na kuzikomboa ardhi zao kutoka kwa adui Mzayuni. Mkuu wa Ofisi ya Kiasia ya Harakati ya Muqawama ya Palestina (Hamas) amesema kuwa, kushiriki pakubwa na siku zote Wapalestina katika msikiti Mtukufu wa al Aqswa kwa ajili ya Sala kumetoa pigo kwa njama mbovu za adui Mzayuni za kutaka kuuhodhi msikiti huo na kuugawa baina ya Waislamu na Wayahudi. Khalid Mash'al ametaka pia kufanyiwa marekebisho muundo wa Harakati ya Ukombozi ya Palestina ili kuipa tena itibari.