EU yataka Saudia iwekewe vikwazo vya silaha
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i1924-eu_yataka_saudia_iwekewe_vikwazo_vya_silaha
Bunge la Ulaya limepasisha azimio la kutaka Saudi Arabia iwekewe vikwazo vya silaha kutokana na vikosi vya utawala wa Aal-Saud kushadidisha hujuma zake dhidi ya taifa la Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 25, 2016 11:59 UTC
  • EU yataka Saudia iwekewe vikwazo vya silaha

Bunge la Ulaya limepasisha azimio la kutaka Saudi Arabia iwekewe vikwazo vya silaha kutokana na vikosi vya utawala wa Aal-Saud kushadidisha hujuma zake dhidi ya taifa la Yemen.

Leo Alkhamisi, wabunge 359 wa bunge hilo wamepiga kura ya kuunga mkono azimio hilo la kuuwekea vikwazo vya silaha utawala huo wa kifalme, kutokana na kile walichokitaja kuwa, Riyadh kushadidisha mashambulio yake dhidi ya raia wasio na hatia nchini Yemen. Wabunge 212 wa Bunge la Ulaya wamepiga kura ya kupinga azimio hilo huku wabunge 31 wakijizuia kupiga kura. Kufuatia kupasishwa azimio hilo, Alyn Smith, Msemaji wa Mashauri ya Kigeni wa European Free Alliance amesema hatua ya kupasishwa azimio hilo imetokana na hujuma za kutisha zinazofanywa na jeshi la Saudia dhidi ya raia wa Yemen. Amesema kuwa: "Saudi Arabia ni mteja mkubwa wa kununua silaha kutoka Uingereza na Ufaransa, na kuna ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa silaha hizo zimetumika katika ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa nchini Yemen, ambapo maelfu ya raia wasio na hatia wameuawa tangu hujuma hizo zianze." Smith amemtaka Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya kutathmini namna vikwazo hivyo vya silaha dhidi ya Riyadh vitakavyotekelezwa. Azimio hilo limepasishwa licha ya Abdulrahman al-Ahmed, Balozi wa Saudia mjini Brussels kufanya lobi za kulitaka Bunge la Ulaya lisilipasishe. Saudi Arabia ilianzisha mashambulizi ya kijeshi nchini Yemen tarehe 26 mwezi Machi mwaka jana 2015, lengo likiwa ni kuisambaratisha harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani Rais mtoro wa Yemen aliyejiuzulu Abdu-Rabuh Mansour Hadi.