Uturuki yateua balozi wake wa utawala haramu wa Israel
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametangaza kuwa Ankara imemteua balozi atakayeiwakilisha nchi hiyo katika utawala haramu wa Israel, miezi michache baada ya pande mbili hizo kutangaza kuhuisha uhusiano wao wa kidiplomasia.
Erdogan amesema serikali yake imemteua Kemal Okem, Mshauri wa Masuala ya Sera za Kigeni wa Waziri Mkuu Binali Yildirim kuwa balozi wa Uturuki huko Israel.
Uteuzi huo wa jana Jumatano umefanyika siku moja baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kumteua Eitan Na’eh, ambaye kwa sasa ni balozi wa Israel mjini London, kuwa balozi wa Tel Aviv mjini Ankara.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Disemba mwaka jana, mwafaka wa kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Uturuki na utawala haramu wa Israel ulifikiwa na maafisa wa ngazi za juu wa Tel Aviv na Ankara mjini Zurich nchini Ujerumani.
Iliarifiwa kuwa, iwapo mwafaka huo utatekelezwa, basi utawala wa Kizayuni wa Israel utaipa Uturuki dola milioni 20 za Marekani, kama fidia kutokana na hatua ya jeshi lake kuua raia wa Uturuki, waliokuwa kwenye meli iliyokuwa na misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza mwaka 2010.
Tukio hilo la kuuawa wanaharakati 9 wa Uturuki na makomandoo wa Israel lilipelekea kuingia doa uhusiano wa pande mbili hizo.