Jeshi la Iraq lakomboa kusini mwa Mosul, magaidi 950 wauawa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i19789-jeshi_la_iraq_lakomboa_kusini_mwa_mosul_magaidi_950_wauawa
Jeshi la Iraq limetangaza kukomboa eneo la kusini mwa mji wa Mosul na kuwaangamiza magaidi zaidi ya 950 wa kundi la kitakfiri la ISIS waliokuwa wanashikilia eneo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 19, 2016 12:13 UTC
  • Jeshi la Iraq lakomboa kusini mwa Mosul, magaidi 950 wauawa

Jeshi la Iraq limetangaza kukomboa eneo la kusini mwa mji wa Mosul na kuwaangamiza magaidi zaidi ya 950 wa kundi la kitakfiri la ISIS waliokuwa wanashikilia eneo hilo.

Afisa wa ngazi za juu katika Polisi ya Iraq, Jenerali Shaker Jodat amesema wanajeshi wamechukua udhibiti wa eneo lenye ukubwa wa kilomita mraba 1,850 kusini mwa Mosul kutoka mikononi mwa magaidi wa ISIS au Daesh sambamba na kuziokoa familia zaidi ya 10,000 zilizokuwa zikishikiliwa mateka hapo.

Aidha Jeshi la Iraq limefanikiwa kuteketeza magari 25 ya magaidi na kutegua mabomu 83 yaliyokuwa yametegwa katika pikipiki sambamba na kuharibu mishipi 92 iliyokuwa imesheheni mabomu ya kutumiwa na magaidi katika hujuma za kujiangamiza.

Magaidi wa ISIS

Siku chache zilizopita Waziri Mkuu wa Iraq Haidar al Abadi alisema kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo wameshaingia katika mji wa Mosul na hivi sasa wanapambana na magaidi wa ISIS ndani ya mji huo.

Operesheni ya kuikomboa Mosul ambayo ni makao makuu ya mkoa wa Nainawa (Nineve) nchini Iraq ilianza tarehe 17 mwezi uliopita wa Oktoba na hivi sasa mwezi mmoja umepita tangu operesheni hiyo ianze huku magaidi wa ISIS wakiendelea kufurushwa kutoka maeneo mengi ya mji huo.