Hamas: Israel inacheza na moto kwa kupiga marufuku Adhana
Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, ameuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel kufuatia amri yake ya kupiga marufuku adhana na kusema sheria hiyo ni sawa na 'kuchezea moto.'
Khaled Meshaal, mkuu wa idara ya kisiasa ya Hamas katika mahojiano na shirika la habari la Anadolu la Uturuki amesema, sheria tata ya kupiga marufuku adhana iliyopendekezwa na Israel imelaaniwa na Wapalestina na Waislamu kote duniani.
Meshaal ameongeza kuwa, Israel imesitisha utekelezwaji sheria hiyo kufuatia hasira za taifa la Palestina ambalo limesema kuzimwa adhana ni mstari mwekundu. Kiongozi huyo wa Hamas amesema hakutakuwa na uthabiti Mashariki ya Kati hadi pale haki za Wapalestina zitakapotambuliwa na Israel kuondoka katika ardhi zote za Palestina inazozikalia kwa mabavu.
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu alisema kuwa anaunga mkono kikamilifu muswada wa sheria ya kupigwa marufuku adhana kwa vipaza sauti misikitini katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeaani vikali mpango huo wa utawala wa Israel kupiga marufuku adhana. Bahram Qassemi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa mpango huo unadhihirisha kuendelea kwa siasa na vitendo vilivyo dhidi ya ubinadamu, ubaguzi, vilivyo dhidi ya haki za binadamu na vya kidhulma vya utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhlumu wa Palestina kwa zaidi ya miongo sita sasa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameitaka jamii ya kimataifa na hasa nchi za Kiislamu kutonyamaza kimya mbele ya hatua hizo za kichokozi na zilizo dhidi ya binadamu za utawala wa Kizayuni na kutotoa mwanya wa kutumbukizwa hatarini utambulisho wa Kiislamu wa Baitul Muqaddas kutokana na hatua kama hizo.