Hamas yaionya Israel kuhusu vita
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imeuonya utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya kuibuka tetesi kuwa utawala huo unapanga kuanzisha vita vipya dhidi ya Ukanda wa Ghaza.
Msemaji wa HAMAS, Mahmoud al-Zahar amesema kuwa Wapalestina watajihami na kukabiliana na hujuma yoyote ile ya Israel katika eneo la Ghaza lenya wakaazi milioni 1.8.
"Hatutafuti sababu ya kukabiliana na Israel, lakini iwapo wataanzisha hujuma, tutapaswa kujihami," amesema Al-Zahar.
Kuna tetesi kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unapanga kuanzisha vita dhidi ya Ghaza kwa lengo la kubomoa njia za chini kwa chini ambazo hutumiwa kuingiza bidhaa za mahitaji ya kibinadamu kutoka Misri. Ghaza imekuwa chini ya mzingiro haramu wa utawala haramu wa Israel tokea mwaka 2007 na wakaazi wa eneo hilo hulazimika kuingiza bidhaa muhimu kama dawa, vyakula n.k kupitia njia za chini ya ardhi.
Al-Zahar amesema Hamas imejenga njia hizo za chini ya ardhi kwa lengo la kutoa huduma za kibinadamu Ghaza.
Afisa huyo wa Palestina pia ameionya Marekani ambayo ni muungaji mkono mkuu wa Israel kuhusu kuupa utawala huo wa Tel Aviv silaha za kisasa na ndege za kivita.
Misri inashirikiana na utawala wa Israel katika kubomoa njia hizo za chini ya ardhi ambazo ni mshipa wa uhai kwa Wapalestina wa Ghaza.