Qassemi: Waziri Mkuu wa Uingereza anajipendekeza kwa nchi za Kiarabu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i21004-qassemi_waziri_mkuu_wa_uingereza_anajipendekeza_kwa_nchi_za_kiarabu
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa vikali matamshi ya chuki dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, yaliyotolewa jana na Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, katika mkutano wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (P)GCC, na kusisitiza kuwa kauli hiyo inalenga kuzifurahisha na kuziridhisha nchi za Kiarabu za baraza hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 08, 2016 04:13 UTC
  • Qassemi: Waziri Mkuu wa Uingereza anajipendekeza kwa nchi za Kiarabu

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa vikali matamshi ya chuki dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, yaliyotolewa jana na Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, katika mkutano wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (P)GCC, na kusisitiza kuwa kauli hiyo inalenga kuzifurahisha na kuziridhisha nchi za Kiarabu za baraza hilo.

Bahram Qassemi amesema nchi zinazochochea machafuko katika eneo haziwezi kuituhumu Iran kuwa inaingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, matamshi ya May yanatokana na changamoto na kipindi kigumu kinachoikabili Uingereza, baada ya nchi hiyo kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya EU.

Theresa May na baadhi ya viongozi wa nchi za Kiarabu

Akizungumza hapo jana katika kongamano la 37 la kila mwaka la Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi mjini Manama nchini Bahrain, Theresa May, Waziri Mkuu wa Uingereza alisema anafuatilia kwa jicho la karibu madai kuwa Iran ni tishio kwa usalama wa Ghuba ya Uajemi na eneo zima la Mashariki ya Kati.

Siku mbili kabla ya kuanza mkutano huo, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilitoa wito wa kukomeshwa uvunjaji wa haki za binadamu unaofanywa na nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi.

May akizungumza katika mkutano wa PGCC mjini Manama, Bahrain

Amnesty ilieleza kusikitishwa kwake na kutoorodheshwa kadhia ya kukanyagwa haki za binadamu katika ajenda za kongamano hilo la kila mwaka la nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi, ambazo ni Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Bahram Qassemi ameongeza kuwa, matamshi hayo ya kujipendekeza ya May yanalenga kuimarisha mauzo ya silaha ya Uingereza kwa nchi hizo za Kiarabu ili kushadidisha mapigano katika nchi za Yemen, Syria, Bahrain, Iraq na nchi nyingine za Kiislamu.