Wapalestina waandamana Ghaza katika maadhimisho ya kuasisiwa harakati ya Hamas
(last modified Fri, 09 Dec 2016 14:16:08 GMT )
Dec 09, 2016 14:16 UTC
  • Wapalestina waandamana Ghaza katika maadhimisho ya kuasisiwa harakati ya Hamas

Makumi ya maelfu ya Wapalestina leo wameshiriki katika maandamano huko Ghaza kuadhimisha mwaka wa 29 wa kuasisiwa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas).

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetangaza kuwa makumi ya maelfu ya raia wa Palestina wakiwemo wanachama na wafuasi wa harakati hiyo wameshiriki katika maandamano makubwa ya kuadhimisha mwaka wa 29 tangu kuasisiwa harakati ya Muqawama ya Hamas, huku wakiwa wamebeba bendera nyeusi za Tauhidi na zile za harakati hiyo. Katika maandamano hayo huko Ghaza, wananchi wa Palestina wamepiga nara  katika kuiunga mkono harakati ya Hamas na kusisitiza kuendeleza mapambano dhidi ya maghasibu wa Kizayuni. Matukio mengi yaliyojiri kufuatia kukaliwa kwa mabavu Palestina mwaka 1948  yaliandaa uwanja wa kuasisiwa Hamas huko Palestina. Hayati Sheikh Ahmad Yasin aliasisi harakati hiyo tarehe 6 mwezi Disemba mwaka 1987.

Sheikh Ahmad Yasin, Mwasisi wa Harakati ya Hamas 

 Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas inaamini kuwa, Israel iliasisiwa  ikiwa ni sehemu ya mpango wa kikoloni wa Magharibi na Wazayuni kwa lengo la kuugawa ulimwengu wa Kiislamu, kuwafukuza Wapalestina katika ardhi yao na kusambaratisha umoja wa Kiislamu. Harakati hiyo inaamini pia kwamba kuendesha jihadi kwa njia tofauti na mbinu mbalimbali ni njia pekee ambayo inaweza kupelekea kukombolewa ardhi za Palestina na kwamba kufanya mazungumzo na Israel ni kupoteza wakati tu na wenzo wa kukiuka haki za Wapalestina.

Tags