Hizbullah ya Lebanon yasifu ushindi mkubwa wa muqawama huko Halab, Syria
Mkuu wa Baraza la Kisiasa la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesifu na kupongeza ushindi muhimu wa kimuqawama katika mji wa Halab (Aleppo) huko Syria.
Ibrahim Amin as Sayyid amesema kuwa, ushindi adhimu wa muqawama uliopatikana katika mji wa Halab huko Syria ni mwana wa ushindi uliopatikana katika vita vya siku 33 vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon. Mkuu wa Baraza la Kisiasa la Hizbullah ya Lebanon ameyasema hayo leo katika marasimu ya kumbukumbu ya mwaka wa kwanza tangu kuaga dunia Sheikh Muhammad Khatum aliyekuwa mwakilishi wa Baraza Kuu la Hizbullah.
Amin as Sayyid ameongeza kuwa, ushindi uliopatikana katika mji wa Halab yaani Aleppo nchini Syria ni mkubwa sana kwa upande wa athari zake kuliko vita hivyo vya siku 33.
Utawala wa Kizayuni wa Israel ulipokea kipigo kutoka kwa wanamuqawma wa Hizbullah katika vita vyake vya siku 33 dhidi ya Lebanon mwaka 2006 na kisha kulazimika kurudi nyuma baada ya kupata hasara na maafa makubwa. Mkuu wa Baraza la Kisiasa la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, ushindi uliopatikana hii leo, umetokana na baraka za mujahidina na damu za mashahidi wa muqawama wa Kiislamu na uongozi wao wa kijeshi na kiusalama.