Bunge la Yemen laidhinisha Serikali ya Wokovu wa Kitaifa
Bunge la Yemen limeidhinisha Serikali ya Wokovu wa Kitaifa, hatua ambayo imehusisha matumaini ya kupatiwa ufumbuzi wa kudumu mgogoro wa kisiasa nchini humo.
Katika kikao cha upigaji kura hapo jana, wabunge wa Yemen walipiga kura kwa wingi kuiunga mkono serikali hiyo mpya. Mara baada ya bunge la Yemen kupasisha Serikali ya Wokovu wa Kitaifa jana Jumamosi, Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema anatumai kuwa serikali hiyo mpya, itarejesha amani na uthabiti katika nchi hiyo ya Kiarabu, mbali na kuzika tofauti zilizopo miongoni mwa makundi mbali mbali ya kisiasa nchini humo.
Mwishoni mwe mwezi uliopita, kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen, Abdul Malik al-Houthi alisema kuundwa serikali mpya ya Wokovu wa Kitaifa ni kwa maslahi ya wananchi wote wa nchi hiyo na ni hatua inayopania kuwapa wananchi hao mamlaka ya kujitawala na kujifanyia maamuzi wao wenyewe.
Serikali hiyo iliyoapishwa Novemba 29, inaongozwa na gavana wa zamani wa Aden, Abdul Aziz Bin Habtoor ambaye amechukua nafasi ya Waziri Mkuu akishirikiana na manaibu watatu na mawaziri 35.
Licha ya hayo, Ismail Ould Sheikh Ahmad, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Yemen amedai kuwa kuundwa serikali mpya ya Wokovu wa Kitaifa nchini humo hakutasaidia kutatua mgogoro wa nchi hiyo.
Hadi hivi sasa mashambulio ya kinyama ya Saudia yameshaua zaidi ya Wayemeni 11,400, kujeruhi mamia ya maelfu ya wengine au kuwaacha bila ya makazi mbali na kuteketeza asilimia 80 ya miundombinu na taasisi za utoaji huduma za lazima kama mahospitali, mashule na taasisi za maji na umeme za nchi hiyo masikini ya Kiarabu.