Silaha za Uingereza zinatumiwa na nchi watenda jinai za eneo
Gazeti la The Guardian limeandika kuwa Uingereza ni muuzaji mkubwa wa pili wa silaha na zana za kijeshi duniani na mdhamini wa silaha nyingi zaidi zinazotumiwa katika vita vinavyoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati.
Gazeti hilo linalochapishwa nchini Uingereza limefafanua kuwa serikali ya London inaziuzia silaha zake nchi kadhaa za Mashariki ya Kati zinazotuhumiwa kutenda jinai za kivita; na hii ni katika hali ambayo Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza inazituhumu nchi hizo kuwa ni wakiukaji wa haki za binadamu.
The Guardian limeashiria mikataba ya uuzaji silaha za Uingereza kwa Saudi Arabia na kuandika kuwa uuzaji silaha katika masoko ya dunia unaitwa biashara ya magendo ya silaha lakini wakati serikali ya nchi fulani inapouza silaha hatua hiyo hupewa jina la kulinda usalama wa taifa au kumsaidia kijeshi muitifaki.
Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti hilo, mwaka uliopita wa 2015 Uingereza iliiuzia Saudia silaha zenye thamani ya dola bilioni moja na milioni 700 na kupokea oda ya kuiuzia nchi hiyo silaha nyingine zenye thamani ya dola bilioni tisa na milioni 200 katika kipindi cha miaka 10 ijayo.
The Guardian limeashiria pia tatizo la nakisi ya bajeti linaloikabili serikali ya Saudi Arabia na kuandika kwa kuhoji, je wananchi wa nchi hiyo wanawataka watawala wao watumie bajeti ya nchi kwa ajili ya kugharamia vita tu?
Kwa mujibu wa gazeti hilo, Saudi Arabia inaanzisha vita vya niaba katika mashariki ya Kati sambamba na kufanya tablighi ya kueneza Uwahabi katika nchi nyingi duniani.../