Trump ateua Mzayuni mwenye misimamo mikali kuwa balozi wa US, Israel
Rais mteule wa Marekani ameteua David Friedman, Mzayuni mwenye misimamo ya kuchupa mipaka kuwa balozi wa Marekani katika utawala haramu wa Israel.
Friedman ambaye amekuwa akiunga mkono ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu, alikuwa mshauri mkuu wa Trump katika masuala ya Israel wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais Marekani.
Mzayuni huyo ambaye amekuwa akipinga mara kwa mara wazo la kutambuliwa rasmi taifa huru la Palestina, amesema atafanya juu chini kuhakikisha kuwa mchakato wa kuuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Quds tukufu (Jerusalem) unafanyika haraka iwezekanavyo.
Haya yanajiri siku chache baada ya Trump kumteua aliyekuwa Kamanda mwandamizi wa jeshi la Marekani Jenerali James Mattis kuwa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo. Mattis mwenye umri wa miaka 66 na ambaye amekuwa akitangaza wazi wazi kuwa haungi mkono makubaliano ya nyuklia ya Iran, ni maarufu nchini Marekani kwa kuendesha operesheni kadhaa katika nchi za Iraq na Afghanistan. Kadhalika afisa huyo wa zamani wa jeshi la Marekani anajulikana kwa jina maarufu la "Jibwa lenye Kichaa" amekuwa akifanya safari za mara kwa mara katika nchi za Kiarabu na utawala haramu wa Israel kwa ajili ya kuendesha njama dhidi ya Iran.
Miongoni mwa maadui wengine wa Uislamu walioteuliwa na Trump ni afisa mstaafu katika Jeshi la Marekani Luteni Jenenrali Michael Flynn aliyeteuliwa na Trump kuhudumu kama mshauri wa usalama wa taifa, licha ya historia yake ya kutoa matamshi makali dhidi ya Uislamu.
Mwengine ni Seneta Jeff Session ambaye alitangaza kuunga mkono msimamo wa Trump wa kuzuia Waislamu kuingia nchini Marekani, aliyeteuliwa kuwa mwanasheria mkuu wa Marekani.