Wananchi wa Bahrain walaani kuhujumiwa nyumba ya Sheikh Issa Qassim
Wananchi wa Bahrain wameandamana kote katika nchi hiyo kulaani hatua ya wanajeshi kuhujumu nyumba ya kiongozi maarufu wa Kiislamu Ayatullah Sheikh Issa Qassim.
Maandamano yalifanyika Jumatano usiku katika maeneo mbali mbali ya nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi kumuunga mkono Sheikh Qassim na kulaani hujuma dhidi ya nyumba yake sambamba na kutaka wafungwa wote wa kisiasa waachiliwe huru.
Mapema Jumatano kuliibuka mapigano wakati wanajeshi wa utawala wa Aal Kalifa walipojaribu kuihujumu nyumba ya Sheikh Qassim katika kijiji cha Diraz. Waandamanaji waliokuwa hapo walijaribu kuwazuia wanajeshi hao na kupelekea machafuko kuibuka.
Kwa muda wa siku 186 sasa wananchi wa Bahrain wamekuwa wakikusanyika nje ya nyumba ya Sheikh Qassim kumuunga mkono tokea Juni 20 wakati utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal Khalifa ulipompokonya uraia mwanazuoni huyo wa Kiislamu menye umri wa miaka 79. Utawala wa Manama unadai kuwa eti anatumikia maslahi ya kigeni, kuunga mkono machafuko na malumbano ya kimadhehebu. Sheikh Qassim amekanusha madai hayo.
Mahakama moja ya Bahrain Jumapili iliyopita iliakhirisha kesi inayomkabili mwanazuoni huyo hadi Januari 5 mwakani.
Ikumbukwe kuwa, Bahrain imekuwa ikishuhudia maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa Aal Khalifa tangu Februari mwaka 2011. Matakwa makuu ya wananchi hao ni kuwepo utawala wa kisheria, kukomeshwa ubaguzi wa kimadhehebu, kufanyika mageuzi ya kisiasa na kuheshimiwa haki za binadamu.