Rais wa Lebanon apongeza nafasi ya Iran katika eneo
Rais Michel Aoun wa Lebanon amepongeza na kusifu nafasi ya Iran katika eneo la Mashariki ya Kati na kubainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imechangia pakubwa kupatiwa ufumbuzi migogoro mbalimbali katika eneo.
Rais Aoun aliyasema hayo jana katika mazungumzo yake na Hossein Jaberi Ansari, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran mjini Beirut na kuongeza kuwa, anatumai kuwa Tehran itaendeleza nafasi na wajibu wake huo katika eneo.
Kuhusu mgogoro wa Syria, Rais wa Lebanon amepongeza mkutano wa pande tatu kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa Iran, Russia na Uturuki na kusisitiza kuwa, mapendekezo ya kikao hicho yatasaidia kuipatia ufumbuzi migogoro inayoikabili Syria, ukiwemo mgogoro wa kisiasa na harakati za magenge ya kigaidi.
Kwa upande wake, Hossein Jaberi Ansari, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayesimamia masuala ya nchi za Kiarabu na Afrika amepongeza kupatiwa ufumbuzi mkwamo wa kisiasa na ombwe la uongozi nchini Lebanon. Amesema mazungumzo ndiyo yaliyoutatua mgogoro wa Lebanon na kwamba kuna haja kwa nchi nyingine za eneo hili kuiga mfano huo katika kuitafutia ufumbuzi migogoro na changamoto za eneo hili.
Baada ya kupita zaidi ya miaka miwili ya mkwamo wa kisiasa, Oktoba 31, Bunge la Lebanon lilifanya kikao chake cha 46 cha upigaji kura na hatimaye kumchagua Michel Aoun mwenye umri wa miaka 81 kuwa rais mpya wa nchi hiyo. Wiki iliyopita, Lebanon ilitangaza baraza jipya la mawaziri linaloongozwa na Waziri Mkuu, Saad al-Hariri, wiki 6 baada ya kuchaguliwa Aoun. Baraza hilo lina mawaziri 30.