Nasrullah: Muqawama utavunja njama za mabeberu
Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah amesema muqawama na kusimama kidete kutasambaratisha njama za madola ya kibeberu na kiistikbari katika nchi za Syria, Iraq na Lebanon.
Akihutubia hadhira iliyokuwa ikiadhimisha kumbukumbu ya kifo cha mwanachuoni wa Kiislamu Sheikh Abdul Naser al-Jabari kwa njia ya televisheni hapo jana, Sayyid Hassan Nasrullah alisema umma wa Kiislamu unakabiliwa na changamoto tele na za hatari na kwamba mapambano tu ndio suluhu ya kuzima njama za maadui wa Uislamu duniani na hususan katika eneo la Mashariki ya Kati.
Sayyid Nasrullah amevitaka vyombo vya habari kuchukua hatua za kukabili njama za kuugawa umma wa Kiislamu kwa misingi ya madhehebu, zinazofanywa na baadhi ya vyombo vya habari na hususan vya Kimagharibi.

Amesema inashangaza namna baadhi ya madola ya Kiistikbari yanavyohalalisha mauaji ya watu wasio na hatia katika baadhi ya maeneo na wakati huo huo yanapinga harakati za muqawama katika maeneo mengine.
Amesisitiza kuwa, wanamuqawama wanataendeleza mapambano hadi wapate ushindi na kuongeza kuwa, kuwaunga mkono wanamapambano hao ni jukumu la kila mtu.
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amefafanua kuwa, mustakabali upo mikononi mwa Wanamuqawama na kwamba, katu wananchi wa Bahrain hawatasitisha mapambano yao dhidi ya utawala wa Aal-Khalifa, namna ambavyo hujuma za utawala wa Aal-Saud dhidi ya Yemen hazijawafanya wananchi wa nchi hiyo maskini wakate tamaa na kufumbia macho kadhia ya Palestina.