Abbas: 2017 utakuwa mwaka wa kujitangazia uhuru Palestina
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas amekaribisha hatua ya hivi karibuni ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kupasisha azimio dhidi ya utawala ghasibu wa Israel na kusema kuwa 2017 utakuwa mwaka wa Palestina kujitangazia uhuru wake.
Akihutubu katika maadhimisho ya miaka 52 tangu kuasisiwa harakati ya Fath ya Palestina katika mji wa Ramallah huko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan hapo jana, Abbas ameukosoa utawala haramu wa Israel kwa kujaribu kupotosha mambo na kuihadaa jamii ya kimataifa kwa kuhalalisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina unazozikaliwa kwa mabavu na kuapa kuwa haitaheshimu azimio hilo la UN.
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameongeza kuwa, lazima utawala bandia wa Israel usitishe ujenzi huo mara moja ili kuepusha kuvurugika zaidi kwa demografia ya Palestina.
Disemba 23 mwaka uliomalizika wa 2016, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 2334 ambalo mbali na kulaani jinai zinazoendelea kufanywa na Israel huko Palestina, linaulazimisha utawala huo ghasibu kusitisha shughuli zote za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.
Azimio hilo ambalo lilipendekezwa na nchi za Malaysia, Venezuela, Senegal na New Zealand, lilipigiwa kura na wanachama 14 wa Baraza la Usalama, huku Marekani ikijizuia kupiga kura.
Mamia ya vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni vimejengwa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel tangu mwaka 1967.