Wasiwasi wa Human Rights Watch kuhusu jinai za Israel
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limebainisha wasiwasi wake juu ya mauaji na jinai zinazotekelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.
Likitoa taarifa hapo jana Jumatatu kuhusiana na suala hilo, shirika hilo limesema kwamba watawala wa ngazi za juu wa Israel wanatuma na kuwashajiisha askari jeshi wao kuwaua kiholela Wapalestina wasio na hatia katika ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo, katika hali ambayo Wapalestina hao kivyo vyote vile si tishio kwa utawala huo. Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadamu limechapisha nyaraka za taarifa zilizotolewa na maafisa wa ngazi za juu wa utawala haramu wa Israel, zinazoonyesha kwamba tokea mwezi Oktoba uliopita hadi sasa, wanajeshi wa utawala huo wametakiwa zaidi ya mara 150 na maafisa wa utawala huo kuwafyatulia risasi kwa njia zisizo za Kisheria Wapalestina wasio na hatia wakiwemo watoto wadogo.
Shirika hilo limesisitiza kwamba utawala huo unapasa kuwaamuru askari wake kutekeleza na kutii sheria za kimataifa. Siku chache zilizopita Moshe Edri kamanda wa polisi katike eneo la Beitul Muqaddas Mashariki aliwapoengeza maafisa wa polisi ambao walifyatua risasi na kumuua shahidi kijana mmoja wa Kipalestina aliyekuwa na umri wa miaka 16 katika eneo hilo.