Saudi Arabia yajaribu kueneza satwa yake barani Afrika
Huku Saudi Arabia ikiendelea kukumbwa na matatizo chungu nzima ya kiuchumi, utawala wa ukoo wa Aal Saud sasa unafuatilia mikakati ya kueneza satwa yake barani Afrika kwa kutia saini mikataba ya kijeshi na nchi za bara hilo.
Hivi karibuni Saudia imetia saini mapatano ya kijeshi na Mauritiani ikiwa ni sehemu ya sera hizo za kujaribu kujipenyeza katika bara la Afrika.
Mohammad bin Abdullah Al Aish, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Saudia, akiwa safarini Nouakchott mji mkuu wa Mauritania, alikutana na Diallo Mamadou Bathia, Waziri wa Ulinzi wa Kitaifa wa nchi hiyo ambapo pande mbili zilitiliana saini mapatano ya ushirikiano wa kijeshi. Mauritania ni nchi iliyo katika eneo la Maghreb, magharibi mwa Afrika Kaskazini. Hali kadhalika mwisoni mwa mwezi Disemba, Saudi Arabia ilitiliana saini mapatano ya ushirikiano wa kijeshi na Sudan.
Djibouti nayo ilitangaza hivi karibuni kuwa Saudi Arabia inapanga kujenga kituo cha kijeshi katika nchi hiyo ndogo iliyo katika eneo la kistratijia la Babul Mandab.
Miongoni mwa nchi 22 ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, 10 ziko katika bara la Afrika ambapo Mauritania, Djibouti na Sudan ni miongoni mwa nchi hizo. Ni wazi kuwa Saudi Arabia inapanga kutumia uanachama wa nchi hizo katika Jumuiya ya Nchi za Kiarbau ili kujipenyeza na hatimaye kuingilia mambo ya ndani ya nchi hizo. Moja ya malengo ya Saudia katika kueneza satwa yake barani Afrika ni kusambaza itikadi ya Uwahhabi katika nchi hizo.

Hakuna shaka kuwa itikadi ya Uwahhabi ni chimbuko na moja ya sababu kuu za kuenea misimamo mikali ya kidini na ugaidi katika bara la Afrika na nchi za Kiislamu kwa ujumla.
Hata baadhi ya wakuu wa nchi za Kiarabu kama vile Tunisia, wametahadharisha mara kadhaa kuhusu kuenea Uwahhabi na kusema Uwahhabi ni chanzo kikuu cha ugaidi.
Lengo jingine la Saudia Arabia kutia saini mapatano ya kijeshi na wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu hasa barani Afrika ni kuunda jeshi la pamoja la Kiarabu. Hata hivyo lengo hilo halijaweza kufanikiwa kutokana na msuguano mkali baina ya Saudi Arabia na nchi muhimu zaidi ya Kiarabu, Misri.
Saudi Arabia inatia saini mikataba ya kijeshi na nchi kama vile Sudan na Mauritania ili iweze kuishinikiza Misri.
Mwishoni mwa mwezi Disemba ujumbe wa ngazi za juu wa kijeshi kutoka Saudia ukingozwa na Abdul Rahman bin Saleh al Banian, Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya ufalme huo ulifika Khartoum na kujadili ushirikiano wa kijeshi baina ya nchi hizo mbili.
Kile ambacho kinapelekea nchi kama vile Mauritania, Sudan na Djibouti kuimarisha uhusiano wa kijeshi na Saudia ni mahitaji ya kifedha ya nchi hizo masikini.
Nchi hizo za Kiarabu-Kiafrika zinajikuribisha kwa Saudia kupata maslahi ya kifedha katika hali ambayo Saudia yenyewe hivi sasa inakabiliwa na matatizo makubwa ya kifedha jambo ambalo limepelekea ufalme huo kuwa na nakisi au upungufu wa bajeti wa takribani dola bilioni 80 mwaka huu.
Katika kukabiliana na hali hiyo mbaya ya kiuchumi, Wizara ya Mafuta ya Saudia imesema mwaka 2017 itaongeza bei ya bidhaa za petroli nchini humo. Mbali na hayo ufalme huo pia umeongeza bei ya huduma mbali mbali kama vile maji na umeme mbali na kupunguza ruzuku ya wafanyakazi wa sekta ya umma na hivyo kusababisha malalamiko ya chini kwa chini.
Kwa hivyo ni wazi kuwa, Saudi Arabia inatumia ushirikiano na mapatano ya kijeshi kujaribu kuzinunua nchi dhaifu za Kiafrika, jambo ambalo bila shaka litapelekea kuongezeka matatizo ya kiuchumi na kuchukiwa zaidi watawala wa ukoo wa Aal Saud ndani ya nchi hiyo.