Jan 08, 2017 03:11 UTC
  • Iraq: Uturuki imeahidi kuondoa askari wake nchini mwetu

Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi amesema kuwa serikali ya Uturuki imeahidi kuondoa askari wake katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.

Al-Abadi aliyasema hayo Jumamosi ya jana mjini Baghdad wakati alipozungumza na waandishi wa habari akiwa pamoja na Binali Yıldırım, Waziri Mkuu wa Uturuki, na kuongeza kuwa, Ankara imeahidi kuondoa askari wake katika kambi ya kijeshi ya Bashiqa huko Mosul, kaskazini mwa Iraq, sambamba na kuheshimu haki ya kujitawala ardhi yote ya Iraq. Ameongeza kuwa,  Iraq na Uturuki zimekubaliana kutoingilia katika masuala ya upande mwingine ikiwa ni kulinda ujirani mwema.

Askari wa Uturuki wakiwa katika eneo la Bashiqa, Mosul, kaskazini mwa Iraq

Kwa upande wake, Binali Yıldırım amesisitiza kuwa, serikali ya nchi yake haitaruhusu hatua  yoyote inayotishia haki ya kujitawala na umoja wa ardhi ya Iraq. Kadhalika Waziri Mkuu huyo wa Uturuki amesema, nchi yake italipatia ufumbuzi wa haraka suala la uwepo wa askari wake katika eneo la Bashiqa. Itakumbukwa kuwa Uturuki ilituma mamia ya askari katika eneo hilo kinyume na sheria, mwishoni mwa mwaka 2015. Serikali ya Ankara ilichukua hatua hiyo kwa kisingizio cha kutoa mafunzo ya kijeshi kwa wapiganaji wa Kikurdi wa Peshmerga kwa lengo la kukabiliana na magaidi wa genge la ukufurishaji la Daesh (ISIS), kitendo ambacho kiliizusha mgogoro wa kidiplomasia baina ya Ankara na Baghdad.

Tags