Mashambulio ya Saudia yaua wanafunzi wanane katika mji mkuu wa Yemen
Wanafunzi wanane wameuliwa shahidi katika mashambulio mapya ya anga yaliyofanywa na ndege za kivita za Saudi Arabia katika mji mkuu wa Yemen Sanaá.
Ndege za kivita za utawala wa Aal Saud leo zimeshambulia skuli moja katika eneo la Nahm lililoko mjini Sanaá ambapo wanafunzi wengine 15 wamejeruhiwa katika shambulio hilo.
Wakati huohuo wakaazi wa mji wa Taiz wameandamana kulalamikia kuendelea kwa mashambulio ya utawala wa Aal Saud na dhiki na mateso wanayohimili wananchi wa nchi hiyo kutokana na hujuma na mashambulio hayo.
Huku wakitoa shaár mbalimbali waandamanaji hao wamesisitiza kuwa hujuma na mashambulio ya Wasaudia na mzingiro wa kidhalimu iliyowekewa Yemen ambavyo vinafanyika kwa uungaji mkono wa fedha na silaha wa baadhi ya nchi za eneo vimewaweka wananchi wa nchi hiyo katika hali ngumu na mbaya mno.
Wananchi wa Yemen katika mji wa Taiz wameashiria pia udharura wa kukabiliana na adui wa Kisaudi kwa ajili ya kuihami nchi na wameutaka Umoja wa Mataifa, baraza lake la usalama na jumuiya za kiraia kuchukua hatua za haraka za kisheria pamoja na maazimio ya kimataifa ili kukomesha jinai za Saudia dhidi ya raia wasio na ulinzi wa Yemen…/