Kunyongwa wapinzani wa utawala wa Aal Khalifa nchini Bahrain
Utawala wa Ukoo wa Aal Khalifa jana Jumapili asubuhi uliwanyonga vijana watatu wapinzani pamoja na kuwa mashirika ya kutetea haki za binadmau yalikuwa yamemuandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa yakitaka vijana walionyongwa kuachiliwa huru mara moja.
Mashirika saba ya kutetea haki za binadamu hivi karibuni yalimuandikia barua Antonio Gutteres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa yakimtaka achukue hatua za kusitisha hukumu ya kunyongowa vijana hao wa Kibahraini ambao walikuwa wakitetea haki na demokrasia nchini humo. Vijana walionyongwa na kufa shahidi ni Sami Mushaima, Abbas Jamil Tahir al-Sami’ na Ali Abdulshahid al-Singace. Mnamo Januari 9 mahakama ya rufaa ya ukoo wa Aal Khalifa ilipinga rufaa ya viajana hao wanaharakati wa demokrasia.
Tokea Februari mwaka 2011, mahakama za Bahrain zimekuwa zikitoa hukumu zisizo za kiuadilifu ambapo idadi kubwa ya wanaharakati wa demokrasia wamehukumiwa kunyongwa. Hukumu hizo zinakiuka kipengee cha 10 cha hati ya kimataifa ya haki za binadamu na kipengee cha 6 cha mapatano ya kimataifa ya haki maalumu za kiraia na kibinadamu.
Hukumu za kunyongwa wapinzani wa kisiasa Bahrain huwa nadra kutekelezwa, lakini mara hii utawala wa kiimla wa Aal Khalifa umepuuza hasira za umma na kuchukua uamuzi wa kutekeleza jinai hiyo ya kuwanyonga vijana ambao hatia yao ni kubainisha upinzani wao kwa utawala huo wa kifalme.
Utawala wa Aal Khalifa umethubutu kutenda jinai hiyo kutokana na kimya cha jamii ya kimataifa pamoja na uungaji mkono kutoka kwa utawala jirani wa ukoo wa Aal Saud ambao nao pia umepata umaarufu kimataifa kwa kuwanyonga wapinzani.
Tokea Februari mwaka 2011, Bahrain imekuwa medani ya mwamko wa Kiislamu wa wananchi dhidi ya utawala wa ukoo wa Aal Khalifa. Kile ambacho wananchi wanamapinduzi wa Bahraini wanataka ni kuwepo uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuja madarakani serikali inayochaguliwa kwa kura za wananchi.
Lakini ukoo wa Aal Khalifa umekandamiza maandamano hayo ya amani ya wananchi kwa mkono wa chuma. Ukandamizaji huo unapata himaya ya moja kwa moja ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ambalo kinara wake ni ufalme katili wa Saudia. Kwa msingi huo maelfu ya wanajeshi wa Saudia wameingia Bahrain kuusaidia utawala wa Aal Khalifa kuwakandamiza wananchi. Hali kadhalika utawala wa kifalme wa Bahrain unapata himaya kubwa kutoka madola ya Magharibi hasa Marekani na Uingereza na pia utawala wa Kizayuni wa Israel.
Saudia inahusika na ukandamizaji wa wananchi wa Bahrain huku yenyewe ikiwa pia inaendelea kuwakadamiza kinyama wapinzani wa ukoo wa Aal Saudi. Duru zinadokeza kuwa maelfu ya raia wa Saudi Arabia hivi sasa wanashikiliwa katika jela za kuogofya za ukoo wa Aal Saudi.
Kwa msingi huo ukoo wa Aal Khalifa unafuata na kutekeleza amri za Saudi Arabia na ndio sababu utawala huo wa Manama ukaanza kuwanyonga kiholela wapinzani.
Ni wazi kuwa uungaji mkono wa Saudia umezipa kiburi tawala za kidikteta katika eneo ambazo zinakandamiza wananchi wanaoandamana kwa amani wakitetea haki zao. Ukoo wa Ali Khalifa sasa umechukua mkondo wa kuwaua wapinzani ili kuibua hofu na woga kwa dhana kuwa jambo hilo litazima sauti ya wapinzani.
Kwa kutekeleza sera za utawa wa kipolisi, ukoo wa Aal Khalifa sasa umeigeuza Bahrain kuwa gereza kubwa kwa wananchi wa nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.
Lakini pamoja na sera zake za ukatili na ukandamizaji ukoo wa Aal Khalifa haujaweza na hautaweza kuzima mwamko wa Kiislamu wa wananchi bali hata wigo wa mwamko huo unazidi kuenea.
Katika fremu hiyo tokea mwanzo wa mwaka huu wa 2017, maeneo mengi ya Bahrain yameshuhudia ongezeko kubwa la maandamano ya wananchi ambao wamechoshwa na utawala wa kiimla wa ukoo katili wa Aal Khalifa. Kushiriki kwa wingi wananchi wa Bahrain katika maandamano ya kutaka mfumo wa demokrasia nchini humo ni jambo linalobaini ukweli huu kuwa, ukandamizaji, ukatili na unyama wa utawala wa Aal Khalifa haujaweza kuvunja azma na irada ya watu wa Bahrain katika kufuatilia malengo matukufu ya mwamko wao.