Utawala wa Bahrain wazidi kukosolewa kwa kuwanyonga wanaharakati
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i23731-utawala_wa_bahrain_wazidi_kukosolewa_kwa_kuwanyonga_wanaharakati
Mkuu wa Vyombo vya Mahakama nchini Iran amelaani hatua ya Bahrain ya kuwanyonga vijana watatu wanaharakati wa nchi hiyo kwa madai bandia ya kuhusika na shambulizi la mwaka 2014, huku akikosoa kimya cha jamii ya kimataifa juu ya ukatili huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 17, 2017 04:06 UTC
  • Utawala wa Bahrain wazidi kukosolewa kwa kuwanyonga wanaharakati

Mkuu wa Vyombo vya Mahakama nchini Iran amelaani hatua ya Bahrain ya kuwanyonga vijana watatu wanaharakati wa nchi hiyo kwa madai bandia ya kuhusika na shambulizi la mwaka 2014, huku akikosoa kimya cha jamii ya kimataifa juu ya ukatili huo.

Akiongea kwenye mkutano na maafisa wa ngazi za juu wa Idara ya Mahakama hapa mjini Tehran jana Jumatatu, Ayatullah Sadeq Amoli Larijani ameyakosoa vikali mashirika yanayojiita kuwa ni ya kutetea haki za bindamu kwa kuendelea kufumbia macho dhulma na ukandamizaji wanaofanywa wananchi wa Bahrain na utawala wa Aal-Khalifa katika nchi hiyo ndogo ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi.

Wanaharakati wa Bahrain walionyongwa na watawala wa Manama

Akiashiria kuwa utawala wa kifalme wa nchi hiyo hautambui haki za msingi za wanachi kama kupiga kura, Ayatullah Larijani amebainisha kuwa muqawama wa wananchi wa Bahrain umewatia kiwewe watawala wa Manama.

Hivi karibuni Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bahram Qassemi alilaani ukatili huo na kusisitiza kuwa, kuendelea kuwekewa mbinyo na mashinikizo wapinzani wa Bahrain kutaitumbukiza nchi hiyo ya katika kinamasi na mkwamo mkubwa wa kisiasa.

Kadhalika siku chache zilizopita, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya mauaji ya kiholela na udikteta alisema, wanaharakati hao wameuawa pasina kuwepo ushahidi juu ya madai wanayolimbikiziwa. Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, utawala wa Manama umewanyonga wanaharakati Abbas al-Samea, Ali al-Singace na Sami Mushaima baada ya kuteswa, kudhalilishwa na kuhukumiwa pasina ushahidi wowote wa kuhusika na vitendo walivyotuhumiwa kufanya.