UN: Kunyongwa vijana wa Bahrain ni dhulma
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, kitendo cha watawala wa Bahrain cha kuwanyonga vijana watatu wa nchi hiyo si cha kiuadilifu.
Msemaji wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa amesema leo kuwa, kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa kuhusu haki za kisiasa na kiraia za watu, ni wazi kwamba kitendo cha vyombo vya mahakama vya Bahrain cha kutoa hukumu ya kunyongwa vijana hao watatu si cha kiuadilifu hata kidogo.
Amesema, vijana hao watatu waliteswa sana na kwamba wakili wao hata hakupewa haki ya kufuatilia kesi yao.
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa Baraza la Haki za Binadamu la Bahrain, familia za vijana hao watatu licha ya kupita muda mrefu wa kutokuwa na taarifa zozote kuhusu vijana hao lakini pia serikali ya Bahrain haikuwapa taarifa kuhusiana na suala la kunyongwa kwao.
Utawala wa ukoo wa Aal Khalifa ulitekeleza adhabu ya kifo dhidi ya vijana watatu wa nchi hiyo siku ya Jumapili.
Madai ya uongo yaliyotolewa na viongozi wa Bahrain dhidi ya vijana hao watatu ya kudai kuwa walishiriki katika mauaji ya polisi mwezi Machi 2014 yamepingwa vikali na jamaa na wanaharakati wa Bahrain.