Utatuzi wa kadhia ya Palestina ni ufunguo wa uthabiti katika eneo
Mshauri wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema utatuzi wa kadhia ya Palestina ni ufunguo wa uthabiti katika eneo la Mashariki ya Kati au Asia Magharibi.
Hussein Sheikhul Islam katika mahojiano na tovuti ya Palestina ya Al Risala amesisitiza kuwa, kuunga mkono Intifadha au mwamko wa Palestina ndio chaguo pekee la kistratijia katika kumaliza tatizo la kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina.
Aidha ameashiria kuhusu Kongamano la Kimataifa la 'Kuunga Mkono Intifadha' ambalo litaanza kesho Jumanne mjini Tehran na kusema kongamano hilo ni mwanzo wa mazungumzo ya Kiarabu na Kiislamu kwa ajili ya maelewano kuhusu kadhia ya Palestina. Sheikhul Islam amesema utawala haramu wa Israel ni adui mkuu na kwamba jitihada zote zinapaswa kutumiwa kukabiliana na utawala huo ghasibu. Aidha amesema Iran inaunga mkono Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas kwa kuwa ni harakati ya kimapambano yenye lengo la kuuangamiza utawala haramu wa Israel.
Mkutano wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina utafanyika tarehe 21 na 22 Februari hapa Tehran kwa kuhudhuriwa na wageni 700 kutoka nchi 80 duniani. Mkutano huo utafunguliwa kwa ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Nara na kaulimbiu kuu ya mkutano huo ni, "Wote kwa Pamoja katika Kuunga Mkono Palestina" na utawaleta pamoja maspika wa mabunge, wabunge, waku wa tume za sera za kigeni katika mabunge, wasomi na wanasiasa wa ngazi za juu, wanaharakati wa kupigania ukombozi wa Palestina na mashirika yasiyo ya kiserikali yenye kutetea Palestina kote duniani.