Wananchi wa Yemen waandamana tena dhidi ya Saudia
Makumi ya maelfu ya wananchi wa Yemen kwa mara nyingine tena wamejitokeza mabarabarani kushiriki maandamano ya kulaani uvamizi na hujuma za kijeshi za utawala wa Saudi Arabia.
Wananchi wa Yemen walioshiriki maaandamano hayo makubwa hapo jana baada ya Sala ya Ijumaa mjini Sana'a, wameutaka Umoja wa Mataifa utekeleza wajibu wake na kuizuia Riyadh kuendeleza jinai zake hizo za kikatili dhidi ya wananchi wasio na hatia wa nchi hiyo ya Kiarabu.
Baadhi ya waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango yenye picha za wahanga wa mashambulizi ya anga ya utawala wa Aal-Saud.
Hii ni katika hali ambayo, sambamba na kufanyika maandamano hayo hapo jana, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Kibinadamu aliitaka Saudi Arabia iziachilie fedha za Yemen ilizozizuia kabla hakujatokea janga la njaa katika nchi hiyo inayokabiliwa na hujuma za kijeshi za Saudia na waitifaki wake.
Stephen O'Brien aliyasema hayo mwishoni mwa safari yake hapo jana nchini Yemen na kusisitiza kwamba, ufumbuzi wa mgogoro wa Yemen hauwezi kupatikana kupitia njia ya kijeshi.
Saudia na waitifaki wake walianzisha hujuma za kila upande dhidi ya Yemen tarehe 26 Machi mwaka 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani kibaraka wao, Abdrabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani wa Yemen ambaye alijiuzulu nafasi hiyo na kukimbilia nchini Saudi Arabia.
Hata hivyo hujuma hizo hazijazaa matunda na badala yake, kwa mujibu wa Jamie McGoldrick, Mshirikishi wa Masuala ya Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, zimeua zaidi ya raia 10,000, kujeruhi wengine 40,000 mbali na kuharibu asilimia kubwa ya miundomsingi ya nchi hiyo maskini.