Russia: Tunapinga pendekezo lolote la kutaka kuiondoa madarakani serikali ya Syria
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa, njama za baadhi ya nchi zenye lengo kupatikana mabadiliko katika suala la mazungumzo ya kutatua mgogoro wa Syria kupitia mabadiliko katika muundo wa serikali ya Damascus, ni suala lisilokubalika.
Sergei Ryabkov, amesema kuwa Moscow inazikaribisha pande tmbalimbali za Syria kwa ajili ya mazungumzo juu ya katiba mpya ya nchi hiyo, lakini haipo tayari kujadili suala la kufanyika mabadiliko katika mfumo wa serikali ya kisheria ya nchi hiyo. Sergei Ryabkov ameongeza kuwa, upande wa Russia unalipa umuhimu suala zima la katiba ya Syria.
Akizungumzia mazungumzo yanayofanyika kati ya makundi mbalimbali ya Syria, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema ushirikiano na ubunifu wa Moscow, Tehran na Ankara ambao ulipelekea kufanyika mazungumzo ya Wasyria mjini Astana, Kazakhstan umeboresha hali ya mambo nchini Syria.
Duru ya kwanza ya mazungumzo ya pande mbalimbali mjini Astana, ilifanyika tarehe 23-24 Januari mwaka huu kupitia ubunifu wa Iran, Russia na Uturuki na yalihudhuriwa na wawakilishi wa serikali na makundi ya wabeba silaha.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa wawakilishi wa serikali ya Syria kukutana moja kwa moja na wawakilishi wa makundi ya wabeba silaha katika mazungumzo hayo. Kabla ya hapo timu za wataalamu wa Russia, Iran na Uturuki na wajumbe wa Umoja wa Mataifa walifanya kikao kingine ambacho kilipelekea kufikiwa makubaliano yanayohusiana na usitishaji vita nchini Syria.