Wamarekani wakiri kuua mamia ya raia Syria, Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i25956-wamarekani_wakiri_kuua_mamia_ya_raia_syria_iraq
Jeshi la Marekani jana lilikiri kuwa limeua raia wa Iraq na Syria katika kampeni inayodaiwa ni ya kupambana na kundi la Daesh kwenye nchi hizo mbili za Kiarabu na Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 05, 2017 04:05 UTC
  • Wamarekani wakiri kuua mamia ya raia Syria, Iraq

Jeshi la Marekani jana lilikiri kuwa limeua raia wa Iraq na Syria katika kampeni inayodaiwa ni ya kupambana na kundi la Daesh kwenye nchi hizo mbili za Kiarabu na Kiislamu.

Shirika la habari la IRIB limenukuu taarifa iliyotolewa na jeshi la Marekani ikisema kuwa, idadi jumla ya raia waliouawa katika mashambulizi ya Marekani nchini Iraq na Syria tangu mwaka 2014 ni 220.

Hata hivyo idadi hiyo ni ndogo sana ikilinganishwa na idadi inayotolewa na watu walioshuhudia na duru zilizoko kwenye medani za vita na zinazofuatilia kwa karibu habari za nchi hizo mbili. 

Kwa mfano takwimu za taasisi ya Airwars zinaonesha kuwa raia wasiopungua 2,463 wameshauliwa katika mashambulizi ya anga ya muungano wa Mrekani huko Iraq na Syria.

 

Muungano huo unaodaiwa kupambana na kundi la kigaidi la Daesh uliundwa wakati wa Rais Barack Obama wa Marekani kwa madai ya kupambana na ugaidi nchini Iraq na Syria.

Hata hivyo ripoti rasmi zinaonesha kuwa, wahanga wakuu wa mashambulizi yanayoongozwa na Marekani kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu na za Magharibi ni raia hasa kwa kuzingatia kuwa nchi hizo ndio waungaji mkono wakuu wa magenge ya kigaidi likiwemo la Daesh (ISIS).