Kuwa mwanachama Palestina wa Jumuiya ya Nchi za Caribbean
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i26310-kuwa_mwanachama_palestina_wa_jumuiya_ya_nchi_za_caribbean
Palestina imekuwa "Mwanachama Mtazamaji" wa Jumuiya ya Nchi za Carribean (ACS). Katika kikao cha Baraza la Mawaziri wa nchi wanachama wa jumuiya ya nchi za eneo la Caribbean kilichofanyika siku ya Jumamosi katika mji mkuu wa Cuba, Havana, Palestina imetangazwa kuwa nchi mwanachama mtazamaji wa jumuiya hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 12, 2017 23:09 UTC
  • Kuwa mwanachama Palestina wa Jumuiya ya Nchi za Caribbean

Palestina imekuwa "Mwanachama Mtazamaji" wa Jumuiya ya Nchi za Carribean (ACS). Katika kikao cha Baraza la Mawaziri wa nchi wanachama wa jumuiya ya nchi za eneo la Caribbean kilichofanyika siku ya Jumamosi katika mji mkuu wa Cuba, Havana, Palestina imetangazwa kuwa nchi mwanachama mtazamaji wa jumuiya hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina Riyadh Al Maliki amesema, kupata uwanachama huo ni matunda ya jitihada zilizofanywa na wizara hiyo mwaka uliopita na kubainisha kwamba jumuiya ya nchi za eneo la Caribbean imeafiki Palestina, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Japan ziwe wanachama watazamaji wa jumuiya hiyo.

Riyadh Al Maliki amebainisha kuwa uwanachama wa Palestina katika jumuiya hiyo yenye nchi wanachama kutoka mabara ya Amerika, Asia pamoja na jumuiya mbalimbali za kimataifa kutakuwa na umuhimu katika kuthibitisha nafasi ya Palestina katika ramani ya dunia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina, Riyadh Al-Maliki

Mkataba wa kuanzisha jumuiya ya nchi za  eneo la Caribbean ulisainiwa nchini Colombia tarehe 24 Julai mwaka1994; na hivi sasa jumuiya hiyo ina nchi wanachama 25 za Amerika ya Latini na eneo la Caribbean. Sekretarieti ya jumuiya hiyo iko Port of Spain, mji mkuu wa kisiwa cha Trinidad na Tobago.

Uungaji mkono wa malengo matukufu ya harakati za kupinga ukoloni katika eneo la Amerika ya Latini na miongoni mwa nchi za eneo hilo una umuhimu maalumu kiasi kwamba mirengo  huru na yenye mielekeo ya utaifa imekuwa daima ikiziunga mkono harakati za kupigania uhuru na ukombozi na kupinga ukoloni. Kwa sababu hiyo akthari ya nchi za eneo la Amerika ya Latini kila mara zimekuwa zikitetea haki za Wapalestina kama ambavyo hapo kabla pia nchi za eneo hilo ikiwemo Chile, Bolivia, Cuba na nyenginezo ziliunga mkono kuundwa nchi ya Palestina na kutambuliwa rasmi katika Umoja wa Mataifa. Hii ni katika hali ambayo kwa upande wa kimasafa na mlingano wa kiutamaduni nchi za eneo la Amerika ya Latini ziko mbali mno na eneo iliko Palestina.

Kitambo nyuma, wabunge wa mabunge ya nchi hizo walitangaza uungaji mkono wao kwa Palestina. Nchi nyengine za eneo la Amerika ya Latini ikiwemo Venezuela nayo pia daima imekuwa ikitilia mkazo kupambana na ukoloni na kusimama imara kukabiliana na dhulma na uonevu. Hili katika hali ambayo nchi nyingi za eneo hilo zimekuwa na zinaendelea kukabiliwa na  mbinyo na mashinikizo ya Marekani kwa sababu ya kufuata siasa hizo za kutetea uhuru na ukombozi. Hivi sasa kutokana na athari za mashinikizo ya Marekani  na vikwazo vya nchi hiyo, nchi nyingi za eneo la Amerika ya Kusini zinakabiliwa na mtikisiko wa kiuchumi. Hata hivyo viongozi wa nchi zinazofuata siasa za mrengo wa kushoto katika eneo hilo wangali wako imara na ngangari katika kushikamana na misimamo yao hiyo.

Kikao cha Havana cha Baraza la Mawaziri

Kwa upande mwengine, utawala wa Kizayuni wa Israel unaoikalia Quds kwa mabavu umekuwa ukijaribu kwa muda mrefu sasa kufanya juu chini ili uwe na satua na ushawishi katika eneo la Amerika ya Latini; hata hiyo licha ya kampeni kubwa zilizofanywa na lobi zenye nguvu za utawala huo katika eneo hilo, kila mara siasa za utawala haramu wa Israel katika eneo la Amerika ya Latini zimeshindwa na kugonga mwamba.

Hivi sasa kupata uwanachama Palestina katika jumuiya ya nchi za eneo la Caribbean sio tu ni ishara nyengine ya uungaji mkono wa nchi za eneo la Amerika ya Latini kwa wananchi madhulumu wa Palestina, lakini suala hilo lina umuhimu wa kipekee zaidi kwa kuzingatia kwamba nchi za eneo hilo ni wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na zina haki za kupiga  kura katika baraza hilo. Kwa muktadha huo zitaweza kwa mara nyengine pale itakapo hitajika kuwasaidia Wapalestina katika uga wa kimataifa. Kitambo si kirefu nyuma viongozi wa nchi za eneo la Amerika ya Latini walizitaka nchi wapenda amani duniani kufanya jitihada za kuhakikisha Wapalestina wanarejeshewa haki zao zote walizoporwa ikiwemo haki ya uhuru na kujitawala na kuuhatimisha ukoloni wa mwisho duniani, yaani ukoloni wa utawala wa Kizayuni wa  Israeil katika Palestina unayoikalia kwa mabavu.../