UN yakosolewa kunyamazia kimya jinai za utawala wa Bahrain
Umoja wa Mataifa umekosolewa vikali kwa kunyamazia kimya jinai zinazofanywa na utawala wa Aal Khalifa dhidi ya wananchi wa Bahrain.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa ripoti jana Jumatano na kusema: "Hali imezidi kuwa mbaya nchini Bahrain katika nusu ya pili ya mwaka 2016. Serikali imezidisha hujuma dhidi ya uhuru wa kujieleza na kukusanyika."
Ripoti hiyo imesema utawala wa ukoo wa Aal Khalifa umepata kiburi zaidi kutokana na kimya cha jamii ya kimataifa kuhusu jinai zake dhidi ya haki za binadamu. Shirika la Human Rights Watch limelitaka Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka kukabiliana na hali mbaya ya haki za binadamu katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.
Tokea tarehe 14 Februari mwaka 2011, Bahrain imekuwa ikishuhudia harakati ya mwamko wa Kiislamu ambapo wananchi wanaandamana kwa amani wakitaka kuwa na haki ya kuwachagua viongozi wao na kuwepo usawa na uadilifu katika nchi hiyo ambayo ni muitifaki mkubwa wa Marekani na Uingereza. Utawala wa kiimla wa Bahrain, kwa msaada wa wanajeshi wa Saudia, unatumia mkono wa chuma kukabiliana na maandamano ya amani ya wananchi.