Marubani wa ndege za kivita za Saudia zinazoua Wayemeni waongezewa mishahara
Sambamba na kushadidi mashambulio ya ndege za kivita za Saudi Arabia dhidi ya maeneo mbalimbali ya Yemen, Baraza la Mawaziri la utawala wa Aal Saud limetangaza kuwa limeongeza mishahara ya marubani wa jeshi la anga la nchi hiyo.
Kituo cha habari cha Ra'ayul-Yaum kimelinukuu shirika rasmi la habari la Saudia likitangaza kuwa Baraza la Mawaziri la nchi hiyo limezifanyia marekebisho sheria za upokeaji mishahara maafisa wa jeshi, na kuongeza kwa asilimia 35 mishahara ya marubani wa jeshi la anga na kwa asilimia 60 mishahara ya marubani wa ndege za kivita.
Hatua hiyo imechukuliwa na utawala wa Aal Saud katika hali ambayo mashambulio ya anga ya nchi hiyo dhidi ya Yemen yameingia mwaka wake wa tatu.
Ikumbukwe kuwa, kwa kushirikiana na nchi kadhaa za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi na baadhi ya nchi za Magharibi, hadi sasa Saudi Arabia imeshafanya mamia ya mashambulio ya anga dhidi ya Yemen kwa lengo la kuvisambaratisha vikosi vya harakati ya Ansarullah, lakini bado haijaweza kufikia lengo hilo.
Tangu mwezi Machi mwaka 2015, utawala wa Aal Saud ulianzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen kwa kisingizio cha kumuunga mkono kibaraka wake AbdRabbuh Mansou Hadi, rais aliyejiuzulu na kuitoroka nchi na ili kuidhoofisha harakati ya Ansarullah.
Uvamizi na hujuma za kijeshi za Saudia na waitifaki wake hadi sasa zimesababisha kuuawa watu wapatao 12,000 wakiwemo wanawake na watoto na wengine wasiopungua 40,000 kujeruhiwa mbali na kuteketeza miundombinu ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu.../