Umoja wa Mataifa walaani siasa za ukandamizaji za utawala wa Saudia
Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu ameukosoa vikali utawala wa Saudi Arabia kwa kukiuka uhuru wa maoni, kuwatia nguvuni kiholela na kuwatesa wanaharakati wa kisiasa nchini humo.
Ben Emmerson, ameyasema hayo katika ripoti maalumu aliyotoa jana kufuatia safari yake ya siku tano nchini Saudia.
Amelaani vikali hatua za viongozi wa utawala wa Aal Saud za kuwatia nguvuni watetezi wa uhuru wa maoni na kuwatesa kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kulinda umoja wa kitaifa wa nchi hiyo.
Emerson ameongeza kuwa viongozi wa Riyadh sio tu hawajaruhusu ufanyike uchunguzi huru kuhusu mashambulio yake ya kijeshi unayoendelea kufanya dhidi ya Yemen ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya familia za raia wa nchi hiyo lakini pia umewatia gerezani waandishi wa habari wengi kwa sababu tu ya kutetea uhuru wa maoni.
Katika ripoti yake hiyo, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu mbali na kuashiria pia kesi nyingi za watu waliotiwa nguvuni na kuwekwa mahabusu bila ya sababu pamoja na utumiaji mbaya wa mamlaka unaofanywa na mahakama bandia za nchi hiyo ameeleza kuwa kosa pekee la wengi kati ya watu hao waliotiwa gerezani ni kukosoa utendaji wa utawala wa Aal Saud.
Amesema, katika safari yake nchini Saudia, amefikishiwa malalamiko mengi ya watu wanaotiwa nguvuni kimakosa, matumizi mabaya ya kanuni za mahakama na kesi nyingi za utesaji ili kuwalazimisha watuhumiwa wakiri makosa.
Aidha ametoa wito wa kuachiwa huru raia 10 wa Saudia ambao amewataja kwa majina akisisitiza kuwa walitiwa nguvuni kiholela kwa sababu tu ya kuukosoa utawala huo wa kifalme.
Emmerson amebainisha pia kuwa licha ya maombi na jitihada kadhaa alizofanya, maafisa wa serikali ya Saudia hawakumruhusu kuonana na yeyote kati ya watu aliowasilisha majina yao kutaka kuwahoji.../