Askofu Mkuu wa Kikatoliki ajiunga na mgomo wa kula kuwatetea Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i28764-askofu_mkuu_wa_kikatoliki_ajiunga_na_mgomo_wa_kula_kuwatetea_wapalestina
Kiongozi mmoja wa ngazi za juu wa Kanisa Katoliki ameamua kususia kula chakula ili kuonyesha mshikamano na uungaji mkono wake kwa Wapalestina waliosusia kula katika magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2025-10-20T07:03:11+00:00 )
May 07, 2017 07:55 UTC
  • Askofu Mkuu wa Kikatoliki ajiunga na mgomo wa kula kuwatetea Wapalestina

Kiongozi mmoja wa ngazi za juu wa Kanisa Katoliki ameamua kususia kula chakula ili kuonyesha mshikamano na uungaji mkono wake kwa Wapalestina waliosusia kula katika magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Gregory III Laham, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki katika maeneo ya Mashariki Yote, Alexandria na Quds Tukufu mwenye umri wa miaka 83 amejiunga na harakati hizo za kususia kula kuonyesha uungaji mkono wake kwa wafungwa wa Kipalestina.

Shirika la habari la al-Wattan linalopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kiarabu limeripoti kuwa, kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Kanisa Katoliki licha ya umri wake mkubwa amechukua hatua hiyo kukosoa ukandamizaji wanaofanyiwa wafungwa wa Palestina katika magereza ya kutisha ya utawala pandikizi wa israel.

Wananchi wa Morocco wakiandamana kuunga mkono Wapalaestina huku wakichoma moto bendera za Israel

Haya yanajiri siku chache baada ya Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon, Salim Al Hooss kujiunga na mgomo huo wa kula, huku akiulaani vikali utawala haramu wa Israel kwa kukiuka sheria za kimataifa kuhusu mateka na wafungwa wa Kipalestina na kutangaza kuwa, ameanza kususia kula ili kuwaunga mkono mateka hao.

Tangu tarehe 17 ya mwezi uliopita wa Aprili zaidi ya Wapalestina 1,700 wanaoshikiliwa kwenye jela za utawala haramu wa Israel walianzisha mgomo usio na muda maalum wa kususia kula chakula kulalamikia vitendo vya ukatili na vya kinyama pamoja na hali mbaya ya huduma na mazingira inayowakabili katika jela hizo.

Mgomo huo unaongozwa na Marwan Al-Barghuthi kwa kaulimbiu ya "Uhuru na Heshima" katika magereza yote ya utawala wa Kizayuni.