Hamas: Tel Aviv inataka kupotosha watu kuhusu mapambano ya Intifadha
(last modified Mon, 14 Mar 2016 07:33:21 GMT )
Mar 14, 2016 07:33 UTC
  • Hamas: Tel Aviv inataka kupotosha watu kuhusu mapambano ya Intifadha

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamasi imetangaza kuwa lengo la mashambulizi yaliyofanywa hivi karibuni na utawala wa Kizayuni wa Israel huko kaskazini mwa Ukanda wa Gaza ni kuwafanya walimwengu wasitilie maanani na kuzingatia mapambano ya Intifadha ya Quds Tukufu.

Raia kadhaa wa Palestina waliuawa shahidi na wengine wengi kujeruhiwa katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa na ndege za kivita za Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza Ijumaa iliyopita.

Ismail Ridhwan ambaye ni miongoni mwa viongozi waandamizi wa Hamas amesema kuhusu mashambulizi hayo kuwa, ni wajibu wa jamii ya kimataifa kusitisha mashambulizi na jinai za Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.

Intifadha ya Quds ilianza mwezi Oktoba mwaka jana ambapo Wapalestina wanaoishi katika ardhi zilizokaliwa kwa mabavu na Israel mwaka 1967 wameanzisha mapambano makali dhidi ya vitendo vya askari wa Israel na walowezi wa Kizayuni vya kuuvunjia heshima mji mtakatifu wa Quds hususan Msikiti wa al Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu.

Wapembuzi wa mambo wanasema serikali ya Waziri Mkuu wa sasa wa Israel, Benjamin Netanyahu imeanzisha vita vya pande zote dhidi ya watu wa Palestina. Baraza la mawaziri lenye mitazamo mikali la Netanyahu limewaua shahidi Wapalestina wanaokaribia 200 katika miezi ya hivi karibu baada ya kuwachochea Wahajiri wa Kiyahudi kuhujumu na kuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa. Maelfu ya Wapalestina pia wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo. Mashambulizi hayo ya walowezi wa Kiyahudi yanafanyika kwa msaada na uungaji mkono wa kikosi maalumu cha jeshi la Israel. Hata hivyo mashambulizi hayo hayakuwavunja moyo Wapalestina bali yamezidisha ari na kuwa chachu na Intifadha mpya ya Quds. Sabamba na hujuma hiyo, Israel imekuwa ikifanya mashambulizi dhidi ya watu wa Gaza. Katika kipindi chote cha miaka 10 iliyopita utawala wa Kizayuni umekuwa ukifanya mashambulizi ya kutisha dhidi ya raia wa eneo lenye msongamano mkubwa la Gaza sambamba na kuwawekea mzingiro wa pande zote kwa shabaha ya kulipiza kisasi dhidi ya harakati ya Hamas. Wiki iliyopita Israel ilizidisha mzingiro huo na kupunguza zaidi kiwango cha bidhaa za ujenzi zinazohitajiwa kwa ajili ya miradi ya ujenzi mpya wa Gaza ambazo ilipangwa kuwa zingepitishwa katika kivuko cha mpakani cha Karam Abu Salim. Hatua hiyo imechukuliwa na utawala wa Kizayuni wa Isarel ili kuwazuia watu wa Ukanda wa Gaza kukarabati nyumba zilizoharibiwa kwa mashambulizi ya ndege na makombora ya utawala huo wa kikatili. Unyama huo mkubwa wa serikali ya Netanyahu unatathminiwa kuwa unafanyika kutokana na nafasi inayolegalega ya Waziri Mkuu huyo wa Israel ambaye anaandamwa na mashinikizo makubwa ya vyama vya upinzani vinavyofanya jitihada za kumuondoa madarakani.

Benjamin Netanyahu amekuwa na utendaji dhaifu na mbaya sana katika siasa za nje, mazungumzo ya Israel na Wapalestina na vilevile katika masuala ya ndani. Kwa kadiri kwamba uchunguzi wa maoni uliofanyika hivi karibuni umeonesha kuwa, umashuhuri wa kiongozi huyo na chama chake cha Likud umepungua kwa kiwango kikubwa baina ya 'Waisraeli.'

Katika mazingira hayo Waziri Mkuu wa Israel ameanza vitimbi vipya katika Ukanda wa Gaza ili kufunika na kupotosha habari zinazohusiana na mapambano ya Intifadha ya watu wa eneo hilo. Mzingiro mkali na wa pande zote wa Ukanda wa Gaza, ukandamizaji dhidi ya Intifadha ya Quds, hujuma na mashambulizi dhidi ya Msikiti wa al Aqsa na mashambulizi ya mara kwa mara ya Wayahudi wenye misimamo mikali dhidi ya raia wa Palestina yote hayo ni kielelezo cha siasa za vita za baraza la serikali ya Israel. Pamoja na hayo viongozi wa harakati ya Hamas wamejibu sera hizo za vita za Netanyahu kwa kusisitiza kwamba jinai hizo hazitapita hivihivi bila ya kupewa majibu.