Trump aunga mkono Saudia katika mgogoro na Qatar
Rais Donald Trump wa Marekani ameunga mkono Saudi Arabia katika mgogoro wake na Qatar na kwa njia isiyo ya moja kwa moja akaituhumu Qatari kuwa inaunga mkono ugaidi.
Katika radiamali yake ya kwanza kufuatia mgogoro mpya wa Saudia na Qatar kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Trump ameandika: "Katika safari yangu Mashariki ya Kati nilitangaza kuwa haiwezekani tena kuvumilia uungaji mkono kifedha idiolojia ya misimamo mikali, na hapo viongozi (wa Kiarabu) wakainyoshea kidole cha lawama Qatar".
Msimamo huu wa Trump unakuja wakati ambao hadi sasa mawaziri wa mambo ya nje na ulinzi wa Marekani wamekuwa wakijitahidi kuonyesha kuwa Washington haiungi mkono upande wowote katika mgogoro wa sasa.
Siku ya Jumatatu utawala wa Saudia uliongoza Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain, Misri, Libya, Maldives na Mauritius katika kukata uhusiano na Qatar. Aidha nchi hizo zimekata uhusiano wa anga, bahari na nchi kavu na Qatar.
Hitilafu baina ya nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi zimeshika kasi baada ya safari ya Trump katika eneo la Mashariki ya Kati wiki chache zilizopita.