Saudia yamuhusisha Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki na ugaidi
Katika kuendelea mgogoro wa nchi za Kiarabu hususan Saudia na Qatar, kanali ya al-Arabiyah ya nchini Saudia imetoa picha ya Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki inayorudi nyuma hadi mwaka 1985, ambapo katika picha hiyo, Erdoğan anaonekana akiwa amenyenyekea mbele ya kiongozi wa chama cha Kiislamu cha 'Gulbuddin Hekmatyar' aliyekuwa akitawala nchini Afghanistan wakati huo.
Kwa mujibu wa kanali hiyo ya al-Arabiya, picha hiyo inathibisha kuwepo mahusiano ya karibu ya Rais Recep Tayyip Erdoğan na Hekmatyar ambaye aliorodheshwa na Marekani katika faili lake nyeusi la ugaidi. Itakumbukwa kuwa, mwezi Aprili mwaka huu, gazeti moja la Uturuki liliandika uamuzi wa Rais Tayyip Erdoğan, Waziri Mkuu Binali Yıldırım na Spika wa Bunge, Ismail Kahraman wa kusitisha amri ya mwaka 2013 ya kuzuia mali za kiongozi wa zamani wa chama cha Kiislamu nchini Afghanistan, Gulbuddin Hekmatyar.

Uamuazi wa kuzuiwa mali za Hekmatyar, aliyekuwa waziri mkuu wa Afghanistan ulikuja baada ya jina lake kuorodheshwa na Washington kuwa miongoni mwa wafadhili wa kundi la al-Qaida na Taleban. Kuonyeshwa picha ya Erdoğan akiwa na Hekmatyar kumetafsiriwa kuwa na maana ya kumuhusisha rais huyo wa Uturuki na ugaidi, suala ambalo linatabiriwa kuwa linaweza kuharibu zaidi mahusiano ya kidiplomasia ya Ankara na Riyadh. Mvutano baina ya Saudia na Uturuki umeongezeka katika siku za hivi karibuni, tangu baadhi ya nchi za Kiarabu zikiongozwa na Saudi Arabia zilipokata mahusiano yao ya kidiplomasia na Qatar, kwa madai kuwa serikali ya Doha inaunga mkono harakati ya wananchi wa Palestina Hamas na harakati ya Ikhwanul Muslimin iliyopigwa marufuku nchini Misri.
Hii ni kwa kuwa baada ya uamuzi huo wa nchi za Kiarabu, Uturuki ilitangaza azma yake ya kutuma jeshi lake kwenda Qatar kwa kile kilichosemwa na serikali ya Ankara kuwa ni kwenda kutoa mafunzo ya kijeshi kwa askari wa Qatar, kitendo ambacho kimewakasirisha mno watawala wa Saudi Arabia.