Qatar: Tuliwakaribisha Taliban mjini Doha kwa matakwa ya Marekani
Afisa wa ngazi za juu wa serikali ya Qatar amesema kuwa, nchi hiyo ililialika kundi la kigaidi la Taliban mjini Doha kutokana na takwa la Marekani ambayo leo, ikiwa pamoja na nchi kadhaa za Kiarabu, inaituhuma Qatar kuwa inaunga mkono makundi yenye misimamo mikali.
Mutlaq al-Qahtani, ambaye ni mshauri mkuu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar katika masuala ya kupambana na ugaidi amesema nchi hiyo iliwakaribisha wakuu wa kundi la Taliban kwa takwa la serikali ya Marekani na kama sehemu ya sera za "mlango wazi" za serikali ya Doha ili kuwezesha mazungumzo, kupatanisha na kurejesha amani.
Kundi la kigaidi laTaliban lilifungua ofisi ya kisiasa mjini Doha mwaka 2013 lakini serikali ya Qatar ilifunga ofisi hiyo hapo baadaye. Inasemekana kuwa, viongozi wa kundi hilo wangali wanaishi mjini Doha.
Qatar imekuwa chini ya mashinikizo makubwa ya nchi za Saudi Arabia, Misri, Imarati na Bahrain ambazo zimekata uhusiano wao wa kisaisa na kiuchumi na nchi hiyo, pamoja na Marekani zinazodai Doha inayaunga mkono makundi yenye misimamo mikali likiwemo la Taliban.
Inaaminiwa kuwa, uamuzi wa Saudia na washirika wake umechochewa na matamshi yaliyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani wakati wa safari yake mjini Riyadh, Saudi Arabia, wiki kadhaa zilizopita.