Jenerali Mzayuni amuonya Netanyahu kuhusu kuichokoza HAMAS
Jenerali mmoja Mzayuni amemuonya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kuhusu siasa zake mbele ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na kusema huko ni kucheza na moto.
Leo Jumapili, shirika la habari la wanafunzi wa vyuo vikuu vya Iran ISNA limemnukuu Meja Jenerali Yaakov Amidror, mkuu wa zamani wa Baraza la Usalama wa Taifa la israel akionya kwamba siasa za Netanyahu dhidi ya HAMAS ni kucheza na moto na ni hatari sana kwa utawala wa Kizayuni.
Amesema, uamuzi wa Israel wa kupunguza kiwango cha umeme unaotumwa katika Ukanda wa Ghaza una maana ya kuwaongezea mashinikizo wakazi wa eneo hilo na kuzidi kuwaweka katika maisha magumu.
Amesisitiza kuwa, ingawa Israel inalihesabu suala la kuwaweka katika mazingira magumu wananchi wa Ghaza kuwa ni fursa nzuri ya kuishinikiza HAMAS na kuilazimisha iache kujiimarisha kijeshi, lakini mashinikizo hayo hayaizuii HAMAS kujiimarisha kijeshi, bali yanazidi kuishawishi harakati hiyo iingie vitani, vita ambavyo ni muhali kutabiri matokeo yake.
Naye Alon Ben-David, mchambuzi wa masuala ya kijeshi wa utawala wa Kizayuni amesema kuwa, uamuzi wa kupunguza kiwango cha umeme unaotumwa katika Ukanda wa Ghaza ni wa kipumbavu.
Ukanda wa Ghaza umezingirwa kila upande na Israel ambayo imefunga njia zote za kuingia na kutoka kwenye ukanda huo tangu mwaka 2007 wakati HAMAS iliposhinda kwenye uchaguzi. Hata umeme wa ukanda huo unatoka katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni. Hivi sasa Israel imeamua kupunguzwa kiwango cha umeme huo kwa asilimia 40.