Ujerumani: Masharti iliyopewa Qatar ni ya kichochezi sana
(last modified Tue, 27 Jun 2017 07:46:59 GMT )
Jun 27, 2017 07:46 UTC
  • Ujerumani: Masharti iliyopewa Qatar ni ya kichochezi sana

Ujerumani imeyataja kuwa ya kichochezi sana masharti iliyopewa Qatar kabla ya kutatulwa mgogoro wake na nchi nne za Kiarabu zinazoongozwa na Saudi Arabia.

Akizugumza Jumatatu mjini Berlin, Naibu Kansela wa Ujerumani ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Sigmar Gabriel ameongeza kuwa baadhi ya matakwa hayo yanakiuka mamlakaya kujitawala Qatar.

Ikumbukwe kuwa Juni tano, Saudi Arabia, Bahrain, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu zilikata uhusiano wa kidiplomasia na Qatar na pia kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa nchi kavu, angani na baharini. Nchi hizo zimedai kuwa Qatar inaunga mkono ugaidi na kuvuruga uthabiti katika eneo madai ambayo wakuu wa Doha wameyakanusha. Kati ya masharti iliyopewa Qatar ili uhusiano wake na nchi hizo urejee katika hali ya kawaida ni kufunga kanali yake ya televisheni ya Al Jazeera, kufunga kituo cha kijeshi cha Uturuki nchini humo, kupunguza kiwango cha uhusiano na Iran na kusitisha ushirikiano na harakati ya ukombozi wa Palestina, Hamas.

Emir wa Qatar

Qatar imekataa kutekeleza matakwa hayo na kusema nchi hizo zinazoongozwa na Saudia zinataka kuiadhibu kwa kufuatia sera huru za kigeni.

Iran imetoa wito wa kuwepo mazungumzo kati ya nchi hizo za Kiarabu zinazozozana huku ikituma shehena za chakula nchini Qatar kila siku kwa msingi wa ubinadamu baada ya Saudia kufunga njia zote zilizokuwa zikitumiwa kufikisha chakula na bidhaa za dharura nchini humo.

 

 

Tags