Wafungwa wa Bahrain katika jela ya Jaw wapaza sauti wakiomba msaada
Wafungwa waliopo katika jela ya Jaw nchini Bahrain wamewaomba raia wa nchi hiyo wawanusuru na dhulma na mateso wanaofanyiwa na watawala wa Aal Khalifa kufuatia siasa za ukandamizaji zinazotekelezwa kila uchao na utawala wa Bahrain.
Wafungwa katika jela hiyo wametuma ujumbe wao wakitaka kukomesha haraka mateso na vitendo viovu wanavyofanyiwa na utawala wa Aal Khalifa na vilevile ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu hususan katika jela kuu ya Jaw.
Karibu wafungwa elfu nne wanaishi katika mazingira magumu na mateso wanayopewa na walinzi wa jela huko Bahrain.
Ujumbe wa wafungwa hao umeongeza kuwa, utawala wa Aal Khalifa unawabana wafungwa hao hata wakati wa kwenda msalani na kadhalika.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zaid bin Raad Hussein amesema kumewasilishwa taarifa za mashtaka mengi kuhusu mateso na vitendo vya ukandamizaji vinavyofanywa kwenye jela hiyo kubwa ya Bahrain na ametoa wito wa kuundwa kamati huru ya kuchunguza malalamiko ya wananchi wa Bahrain.