Qatar yatangaza jeshi lake liko tayari kwa ajili vita
Waziri wa Ulinzi wa Qatar amesema jeshi la nchi hiyo liko tayari kuilinda nchi hiyo endapo itakabiliwa na chokochoko tarajiwa za maadui.
Khalid al-Attiyah Waziri wa Ulinzi wa Qatar amesema nchi yake iko katika hali ya tahadhari kamili kijeshi kwa ajili ya kuhijami.
Akizungumza mapema Jumapili usiku katika mahojiano na Televisheni ya Sky News ya Uingereza, al-Attiyah amesema: "Nchi ambazo zimeiwekea Qatar mzingirio zinapanga kumpinduia Amiri wa nchi hiyo Tamim bin Hamad Aal Thani. Ameongeza kuwa, anataraji kuwa mgogoro uliojitokeza baina ya nchi yake na baadhi ya tawala za Kiarabu zikiongozwa na Saudi Arabia hautafika katika makabiliano ya kijeshi.
Wakati huo huo Mohammad bin Abdul Rahma Aal Thani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar amesema nchi yake iko imara na wala haina hofu yoyote kuhusu uvamizi wa kijeshi wa Saudia.
Itakumbukwa kuwa, utawala wa Saudia Arabia iliziongoza Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Misri Jumatatu ya 5 mwezi Juni mwaka huu kukata uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar na kisha zikaizingira kiuchumi nchi hiyo.
Si hayo tu lakini pia Saudi Arabia na waitifaki wake tarehe 23 mwezi Juni mwaka huu ziliipa Qatar masharti yenye vipengee 13 zikisema kuwa, suala la kurejesha uhusiano kati ya nchi hizo na Qatar litategemea namna Doha itakavyotekeleza masharti yao hayo. Qatar imesema wazi kuwa masharti hayo hayatekelezeki kwani yanalenga moja kwa moja utambulisho, hadhi na haki ya kujitawala nchi hiyo.