Taarifa ya pamoja ya Saudia na waitifaki wake dhidi ya Qatar
(last modified Fri, 07 Jul 2017 03:58:22 GMT )
Jul 07, 2017 03:58 UTC
  • Bendera za nchi nne za Kiarabu zilizoiwekea vikwazo Qatar
    Bendera za nchi nne za Kiarabu zilizoiwekea vikwazo Qatar

Saudi Arabia na waitifaki wake zimetoa taarifa ya pamoja na kudai kuwa hatua ya Qatar ya kukataa masharti ya nchi nne za Kiarabu zilizoiwekea vikwazo vya kila namna nchi hiyo inaonesha nia ya Doha ya kuhatarisha usalama na utulivu wa eneo hili.

Jumatatu ya tarehe 5 Juni, nchi za Saudi Arabia, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu yaani Imarati na Bahrain zilitoa taarifa tofuati na kutangaza kukata uhusiano wao wa kila upande ukiwemo wa kidiplomasia na Qatar. Tarehe 23 Juni nchi hizo ziliipa masharti 13 Doha ya kurejesha uhusiano wa kawaida na nchi hizo na kuiwekea muda maalumu Qatar wa kuhakikisha imetangaza kukubaliana na masharti hayo bila ya kuhoji chochote.

 

Hata hivyo Qatar imeyahesabu masharti hayo kuwa yanalenga moja kwa moja kwenye uhuru wa kujitawala nchi hiyo. Wataalamu mbalimbali nao walisema kuwa masharti hayo hayatekelezeki na inaonekana yalitolewa kwa makusudi ili kuifanya Doha ishindwe kuyatekeleza na hivyo nchi hizo nne za Kiarabu zipate kisingizio cha kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya Qatar. Kama ilivyotarajiwa, hatimaye serikali ya Doha iliwasilisha rasmi msimamo wake wa kukataa masharti hayo.

Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa na nchi nne za Saudi Arabia, Misri, Imarati na Bahrain baada ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo kukutana huko Cairo Misri imedai kuwa masharti ya nchi hizo kwa Qatar eti yalilenga kupambana na ugaidi na kulinda usalama wa nchi za Kiarabu na wa kimataifa.

Mgogoro baina ya nchi hizo za Kiarabu umechochewa na safari ya tarehe 20 Mei 2017 ya rais wa Marekani, Donald Trump mjini Riyadh Saudi Arabia ambapo Saudia iliahidi kununua silaha za mabilioni ya dola kutoka kwa Marekani.

Tags