Misri yaweka vikwazo vipya dhidi ya Qatar
Misri imeifungia Qatar njia zote za majini zinazotumiwa na meli za Qatar isipokuwa mfereji wa Suez.
Katika mwendelezo wa kuiwekea vikwazo Qatar sambamba na Saudi Arabia, Misri imezizuia meli za Qatar kutumia bandari zake. Hata hivyo imeiruhusu Doha kutumia mfereji wa Suez kupitishia meli zake.
Mkuu wa Mamlaka ya Mfereji wa Suez, Mohab Mamish ambaye pia ni Mwenyekiti wa Ukanda wa Kiuchumi wa mfereji huo amesema kuwa, sheria zinazohusiana na safari katika mfereji wa Suez zinafungamana na makubaliano ya kimataifa yaliyosainiwa na Cairo. Afisa huyo wa Misri ametilia mkazo kuwa, meli za Qatar zitazuiwa kutumia bandari za Misri na ukanda wa kiuchumi wa mfereji wa Suez.
Makumi ya meli hupita katika mfereji wa Suez kila siku na kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa, Cairo haiwezi kuzizuia meli kupita katika mfereji huo.
Nchi nne yaani Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri ziliiwekea vikwazo Qatar tangu tarehe 5 mwezi Juni mwaka huu. Nchi hizo nne za Kiarabu tarehe 23 mwezi Juni mwaka huu ziliipatia Qatar masharti yenye vipengee 13 ili keresha uhusiano wao na nchi hiyo, matakwa ambayo hata hivyo yemepingwa na Doha ikisema kuwa hayana mlingano, si ya kimantiki na hayayowezi kutekelezeka.